Jamii FM
Jamii FM
5 March 2025, 21:50 pm

Kila ifikapo March 8 ya kila mwaka Dunia huadhimisha siku ya Mwanamke Duniani dhamira ikiwa kutambua mchango mkuu unaotolewa na Mwanake katika jamii hivyo kuelekea siku hiyo shirika la SDA,TASA na SSDM wamefanikisha kupeleka ujumbe juu ya haki ,usawa na changamoto za ukatili wa kijinisia kupitia tamasha la michezo lililo wahusisha wanafunzi wa shule mbili za sekondari
Na Musa Mtepa
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Shirika la Michezo la Sports Development Aid (SDA) mkoani Mtwara limefanya tamasha la michezo kwa wanafunzi wa shule za sekondari za Chuno na Likombe likiwa kama sehemu ya kutoa elimu kuhusu haki za wanawake, uimarishaji wa usawa wa kijinsia, na kuboresha nafasi za wanawake katika jamii.
Akizungumzia tamasha hilo March 4, 2025, Mwakilishi wa SDA, Jacklini Mpunjo, amesema kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na mashirika matatu wameandaa tamasha hilo kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu haki za wanawake na kutetea usawa wa kijinsia mkoani Mtwara na nchini kwa ujumla.

Jacklini ameishukuru serikali kwa ushirikiano mkubwa, hasa kwa viongozi wa kata na halmashauri, ambao wameunga mkono na kuchangia mafanikio ya tamasha hili.
Kwa upande wake, John Daniel, Mkurugenzi wa Shirika la TASA, lililoshirikiana katika tamasha hili, amesema watoto wa kike na wa kiume wamehusika kwa pamoja katika michezo mbalimbali. Lengo kuu likiwa ni kuelimisha jamii kuhusu namna ya kuepuka vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kutumia watoto kama chombo cha kufikisha ujumbe.
Latifa Hamisi, mwanasaikolojia kutoka taasisi ya Street Sports Disability Mental (SSDM), ameeleza kuwa michezo hiyo imelenga pia kuimarisha afya ya akili na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa wanawake katika jamii.
Latifa amesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa mtoto wa kike ili aweze kufikia malengo yake na kuboresha hali ya afya ya akili katika jamii.

Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani tarehe 8 Machi 2025, Latifa Hamisi amehamasisha wanawake wenye sifa kujiandaa kushiriki katika uchaguzi na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, akisema ni muhimu kuwa na uwakilishi wa wanawake katika nyadhifa za juu.
Tamasha hili limeratibiwa na mashirika matatu yasiyo ya kiserikali: SDA, TASA, na SSDM, likiwa na lengo la kuhamasisha jamii kuhusu haki za wanawake, kutambua changamoto za kijinsia, na kuimarisha usawa katika jamii kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani.
