Jamii FM

Wahitimu Mtwara Ufundi wachangia ujenzi wa msikiti Mtwara

5 January 2026, 18:10 pm

Eneo linalotarajiwa kujenga Msikiti katika mtaa wa Shule ya msingi Majengo kata ya Tandandika Manispaa ya Mtwara Mikindani (Picha na Musa Mtepa)

Wanafunzi waliowahi kusoma Shule ya Sekondari Mtwara Ufundi wamechangia shilingi 525,000/= kwa ajili ya ujenzi wa Msikiti wa mtaa wa Shule ya Msingi Majengo, Manispaa ya Mtwara

Na Musa Mtepa

Wanafunzi waliowahi kusoma Shule ya Sekondari Mtwara Ufundi iliyopo Manispaa ya Mtwara ya Mikindani, wamechangia jumla ya shilingi laki tano na elfu ishirini na tano (525,000/=) kwa ajili ya ujenzi wa msikiti wa mtaa wa shule ya msingi Majengo.

Akizungumza leo Januari 5, 2026 mara baada ya kukabidhi mchango huo katika eneo linalotarajiwa  ujenzi wa Msikiti huo, mwanajumuia wa wanafunzi hao, Hamdani Swalehe Amlima, amesema kuwa wao kama wadau waliamua kuwashirikisha wenzao waliowahi kusoma Shule ya Sekondari Mtwara Ufundi ili kuona namna wanavyoweza kusaidia ujenzi huo, hatua iliyowezesha kupatikana kwa mchango huo.

Sauti ya Hamdani Swalehe Amlima – Mwanajumuia
Mwanajumuia ya wanafunzi waliowahi kusoma shule ya Sekondari Mtwara Ufundi akikabidhi fedha shilingi 525,000/= kwa mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Msikiti(Picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Msikiti huo, Mzee Musa Napinda, ameishukuru jumuia hiyo kwa mchango wao akisema kuwa fedha hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa katika hatua za awali za ujenzi wa Msikiti huo.

Aidha, Mzee Napinda ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau wa maendeleo pamoja na waumini mbalimbali kujitokeza kuchangia ujenzi wa Msikiti huo ili kuwasaidia waumini wa Kiislamu katika eneo hilo kupata sehemu ya karibu ya kufanyia ibada.

Sauti ya Mzee Musa Napinda – Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Msikiti

Nao baadhi ya viongozi na waumini wa mtaa wa Shule ya Msingi Majengo wameishukuru jumuia hiyo pamoja na Diwani wa kata hiyo kwa kuhamasisha na kufanikisha upatikanaji wa mchango huo, huku wakiomba taasisi, wadau na waumini wengine kujitokeza ili kufanikisha ujenzi wa Msikiti huo.

Sauti ya waumini na viongozi wa mtaa unaojengwa Msikiti
Mhe; Diwani wa kata ya Tandika Al-Hajji Haroun Selemani Haroun akiwa na baadhi ya viongozi wa kamati ya ujenzi wa Msikiti wa mtaa wa Shule ya Msingi Majengo(Picha na Musa Mtepa)

Naye Diwani wa Kata ya Tandika, ambako Msikiti huo unatarajiwa kujengwa, Al-Hajji Haroun Selemani Haroun maarufu kama Chai Jaba, amewashukuru wakazi wa mtaa wa Shule ya Msingi Majengo pamoja na wanajumuia wa Mtwara Ufundi kwa moyo wao wa kujitolea na kushiriki katika kutoa sadaka hiyo (Swadakati Jaria).

Sauti ya Al-Hajji Haroun Selemani Haroun – Diwani wa Kata ya Tandika