Jamii FM
Jamii FM
04/03/2026, 16:05

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ahimiza ushirikiano wa TPDC na viongozi wa Mtwara katika miradi ya CSR, huku akisisitiza ajira na uwezeshaji wa wananchi kwenye miradi ya gesi asilia
Na Musa Mtepa
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na kampuni zinazojihusisha na shughuli za gesi asilia mkoani Mtwara kushirikiana kwa karibu na viongozi wa maeneo husika wakati wa utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Ameyasema hayo Februari 27 na 28, 2026 alipokuwa katika ziara ya kikazi, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na viongozi wa vijiji, madiwani, wabunge na halmashauri ili miradi inayotekelezwa iendane na gharama halisi pamoja na thamani ya fedha inayowekezwa na Serikali.
Aidha, Mhe. Ndejembi ameagiza kuendelezwa kwa uwezo wa Watanzania, hususan wa maeneo yanayozunguka miradi ya gesi, ili waweze kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma hatua hiyo inayolenga kuongeza mzunguko wa fedha na kukuza uchumi wa maeneo husika.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya CSR, Mjiolojia Mwandamizi ambaye pia ni Meneja wa Mradi wa Utafutaji wa Mafuta na Gesi katika Kitalu cha Lindi–Mtwara, Shaidu Nuru, amesema kuwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo wamefanikiwa kurejesha faida kwa jamii kupitia miradi mbalimbali.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na ununuzi wa mabati kwa ajili ya Soko la Kijiji cha Mkwajuni Juu, ujenzi na ukarabati wa viwanja vya shule, uboreshaji wa barabara za kuunganisha vijiji, pamoja na kusaidia sekta ya afya katika maeneo yanayozunguka mradi.

Shaidu Nuru amesema lengo kuu la mradi wa Lindi –Mtwara ni kutafuta rasilimali za mafuta na gesi asilia ili kuhakikisha taifa linakuwa na nishati ya kutosha, hatua itakayochochea maendeleo kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa mbali na manufaa ya moja kwa moja yatokanayo na upatikanaji wa nishati, pia kuna fursa mbalimbali kwa jamii zinazoguswa na mradi huo, ikiwemo ajira. Amesema waliendesha kampeni maalum kuhakikisha kazi zote zisizohitaji utaalamu wa hali ya juu zinafanywa na wakazi wa maeneo husika, kama ilivyotekelezwa wakati wa mradi huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Mhe. Arif Premji, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya gesi asilia mkoani Mtwara huku akibainisha kuwa miradi hiyo pamoja na ile ya CSR imekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha huduma za kijamii na maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.
