Jamii FM

Mahakama yaendelea kuimarisha utoaji wa haki Mtwara

4 February 2026, 06:50 am

Mhe.Edwin Kakolaki Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara akihutubia katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini iliyofanyika viwanja vya Mahakama kanda ya Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara imesema inaendelea kuimarisha uwezo wake ili kuhakikisha utoaji wa haki kwa wakati kama sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kauli hiyo imetolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika Mtwara.

Na Musa Mtepa

Katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mahakama kwa kushirikiana na Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uwezo wake ili kusimamia utoaji wa haki kwa wakati kwa taasisi, mashirika na wananchi nchini.

Hayo yameelezwa Februari 2, 2026 na Mheshimiwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Edwin Kakolaki, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara.

Sauti ya 1: Edwin Kakolaki – Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara

Mheshimiwa Jaji Kakolaki amesema kuwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, muhimili wa Mahakama una nafasi muhimu katika kujenga taifa lenye haki, amani, usalama na utulivu kwa kujenga mazingira salama ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

Sauti ya 2: Edwin Kakolaki – Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara
Watumishi wa Mahakama wakiwa katika viwanja Mahakama kuu kanda ya Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Aidha, Jaji Kakolaki amesema Mahakama imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika matumizi ya teknolojia, hatua inayochangia kuongeza ufanisi na kasi ya utendaji kazi ikilinganishwa na miaka ya nyuma, jambo linalosaidia wananchi kupata haki kwa wakati.

Sauti ya 3: Edwin Kakolaki – Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara
Mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdala Mwaipaya akimkaribisha mkuu wa mkoa wa Mtwara tayari kwa kutoa salamu za mkoa katika maadhimisho hayo(Picha Musa Mtepa)

Akitoa salamu za maadhimisho hayo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Mkoa wa Mtwara, Lightness Kikao, amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo imebeba uzito mkubwa kwa kuwa inaakisi ukweli kwamba hakuna maendeleo ya kweli bila uwepo wa haki, utawala wa sheria na misingi ya utawala bora.

Sauti: Lightness Kikao – Makamu Mwenyekiti, TLS Mkoa wa Mtwara
Makamu Mwenyekiti, TLS Mkoa wa Mtwara Lightness Kikao akitoa akitoa salamu za TLS (picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrik Sawala, ambaye alikuwa mgeni maalumu katika maadhimisho hayo, amesema utoaji wa haki kwa wakati kwa wananchi utadumisha amani na utulivu katika mkoa wa Mtwara na taifa kwa ujumla, hali itakayowapa wananchi fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa amani.

Sauti: Kanali Patrik Sawala – Mkuu wa Mkoa wa Mtwara
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanal Patrik Sawala akitoa salamu za mkoa katika maadhimisho ya siku sheria nchini (Picha na Musa Mtepa)