Wadau wa mazingira Mtwara waiomba serikali kupunguza bei ya mitungi ya gesi ya kupikia
3 June 2024, 18:45 pm
Serikali na makampuni yanayotengeneza na kuuza mitungi ya gesi iangalie namna nyingine ya kutengeneza mitungi midogo yenye gharama nafuu ili mwananchi wa hali wa chini aweze kuinunua na kutumia ikiwa kama njia ya kupunguza matumizi ya nishati chafu ya kupikia .
Na Musa Mtepa
Wadau wa mazingira mkoani Mtwara wameiomba serikali kuharakisha mchakato wa matumizi ya nishati safi ya kupikia Pamoja na kupunguza gharama za nishati hiyo ili kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni ambao umekuwa ukichangia kwa asilimia kubwa uharibifu wa mazingira.
Wakizungumza Juni 2,2024 kwenye kongamano la vijana kuhusu fursa za kimazingira lilizofanyika katika chuo cha Stella Maris (STEMCO) Mtwara wadau hao wamesema kuwa hali ya kiuchumi ya wananchi wengi kutokuwa mzuri kunawasababishia kuendelea kutumia nishati chafu (kuni na mkaa)hivyo ni wakati wa serikali kuona haja ya kusimamia na kupunguza gharama ya manunuzi ya gesi .
Aidha Petronila Fabian ameishauri serikali kuona namna inaweza kuendeleza mpango wake wa matumizi ya gesi asilia majumbani hasa kwa maeneo ya vijijini ambako kwa kiasi kikubwa uharibifu na uchafuzi wa mazingira umekuwa ukifanyika .
Naye Daktari Maria Manase kutoka chuo cha Afya na Sayansi shirikishi Mtwara (COTC) amesema Pamoja na upatikanaji wa mitungi ya gesi makampuni na serikali itengenezwe namna bora ya upatikanaji wa gesi ya ujazo mdogo ambayo itanunuliwa kwa bei nafuu ili kumsaidia mwananchi wa hali ya chini kufikia gharama zake.
Stella Joseph na Felista Mapunda wamesema ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi jamii haina budi kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia Pamoja na kutoa elimu juu ya matumizi nishati hiyo ili isileta madhara kwa mtumiaji.
Kwa upande wake meneja wa baraza la taifa la uhifadhi na usimamizi wa mazingira (NEMC) kanda ya kusini Mhandisi Boniphace Guni amesema serikali imejipanga kuja na mkakati wa kuwa na nishati safi nchini ambao umezinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassani wenye lengo la kutumia nishati safi kupitia rasilimali zilizopo nchini.