Jamii FM
Jamii FM
02/03/2026, 16:58

Waziri Nanauka amewahimiza vijana kujiandaa kuchangamkia fursa za maendeleo wakati wa uzinduzi wa Vijana Platform Mtwara
Na Musa Mtepa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Mhe. Dkt. Joel Nanauka, amewataka vijana kuwa na maandalizi madhubuti ili kuchangamkia fursa zinazotolewa na wadau mbalimbali pamoja na wizara hiyo.
Ametoa kauli hiyo leo Machi 2, 2026 wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Vijana Platform) mkoani Mtwara, uliofanyika katika viwanja vya Chuo cha Stella Maris, Mtwara.
Waziri Nanauka amesema jukwaa hilo linalenga kufungua ndoto za vijana na kuwawezesha kuchangamkia fursa za maendeleo, akisisitiza kuwa maandalizi ni msingi wa mafanikio.
Akizungumzia shilingi bilioni 200 zilizotolewa na serikali kwa Wizara ya Maendeleo ya Vijana kwa ajili ya kusimamia mikopo ya vijana na wanawake, Waziri Nanauka amewataka vijana kufuatilia taarifa sahihi kupitia ngazi za kata hadi halmashauri ili kufahamu taratibu za mikopo hiyo.
Aidha, Dkt. Nanauka amezielekeza halmashauri zote nchini kuhakikisha vijana wanapewa kipaumbele katika utoaji wa tenda za huduma mbalimbali za kiserikali, ikiwemo shughuli za Mwenge.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Donald Msengi, amesema mkoa umejipanga kuhakikisha vijana wanachangamkia fursa za kiuchumi zikiwemo kilimo, uchumi wa bluu na miradi mingine ya kimkakati inayotekelezwa mkoani humo.
