Kisima cha maji chadhaniwa kuwa na gesi asilia Mtwara Vijijini
1 October 2024, 00:23 am
Hii ni hali inayowashangaza wananchi wengi wa kijiji cha Mnyundo huku fikra zao zikiwa katika uwepo gesi asilia sehemu ambayo maji yanatokea .
Na Musa Mtepa
Wananchi wa kijiji cha Mnyundo, kata ya Ndumbwe, halmashauri ya Mtwara, mkoani Mtwara, wamesema kuwa visima vya maji vimegeuka kuwa sintofahamu baada ya tukio la ajabu.
Wakizungumza na Jamii FM, wananchi hao wamesema hali hii ilianza kutokea baada ya kijana mmoja mwenye tatizo la afya ya akili kufika kisimani hapo kuoga na baada ya kuoga, kijana huyo alishika njiti ya kibiriti na kuiwasha ndipo moto ukaibuka juu ya maji yaliyokuwepo kisimani.
Tukio hili limeendelea kwa zaidi ya miezi mitano, na sasa visima hivyo vimekuwa sehemu ya kivutio kwa watu wanaotaka kujionea wenyewe.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mnyundo Rashidi Musa amethibitisha kuwepo kwa hali hii na kusema ameshapeleka taarifa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na viongozi wa serikali ambapo wataalam wa TPDC walifika na kuchukua vipimo ambavyo hadi sasa bado vinasubiriwa ili kubaini chanzo cha moto na athari zinazoweza kutokea kwa wananchi kutokana na matumizi ya maji hayo.
Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka TPDC, Ali Mluge, akizungumza kwa njia ya simu, amesema kwamba wamepokea taarifa hizo na tayari wametuma wataalam kufanya tathmini ya kitaalam ili kubaini nini kinasababisha na hivi karibuni watatoa taarifa rasmi.
Hali hii inaonesha umuhimu wa ufuatiliaji wa masuala ya maji na usalama wa jamii, ili kuhakikisha kwamba matumizi ya maji ni salama kwa wananchi.