Jamii FM
Jamii FM
1 April 2026, 15:24

Wananchi wa Mnyahi Mtwara walalamikia kuchelewa kwa ujenzi wa soko licha ya makato ya korosho, wakitupia lawama viongozi wa kijiji na mfumo wa ukusanyaji fedha
Na Musa Mtepa
Wananchi wa kijiji cha Mnyahi, kata ya Milangominne mkoani Mtwara, wameulalamikia uongozi wa kijiji pamoja na Halmashauri ya Mji Nanyamba kwa kuwa kikwazo cha kutokamilika kwa miradi ya maendeleo inayoanzishwa na kijiji hicho, inayotegemea makato ya zao la korosho linalolimwa katika eneo hilo.
Wakizungumza na Jamii FM Radio, wananchi hao wamesema kuwa takribani miaka mitatu sasa imepita tangu walipokubaliana katika mkutano wa kijiji kukatwa shilingi 20 kwa kila kilo moja ya korosho, ili fedha zitakazopatikana ziweze kuwezesha ujenzi wa soko jipya kijijini hapo.

Aidha, wananchi hao wamesema kuwa changamoto inayosababisha kuchelewa kwa ujenzi wa soko hilo ipo katika serikali ya kijiji, wakidai kuwa baadhi ya viongozi hawawajibiki ipasavyo, hususan katika uendeshaji wa mikutano ya kijiji. Pia wameomba viongozi wakuu wa vyama vinavyowaweka madarakani viongozi wa vijiji kuwafuatilia kwa karibu utendaji wao wa kazi baada ya uchaguzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Mnyahi, Hamisi Salumu Mpangu, amesema kuwa changamoto kubwa ya upatikanaji wa fedha hizo kwa wakati na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inatokana na matatizo anayokutana nayo mtendaji wa kijiji katika kutumia mfumo wa NeST, hali inayochangiwa na umri pamoja na uelewa mdogo wa matumizi ya mfumo huo.

Akitolea ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Mnyahi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, Mhe. Hassani Ali Mauji, amesema kuwa fedha hizo hukusanywa awali na MAMCU, na baada ya msimu kumalizika hufanya makusanyo ya pamoja ya halmashauri yote na kuziingiza katika akaunti ya halmashauri. Baadaye, mkurugenzi huzipeleka katika akaunti za vijiji kulingana na kiwango cha fedha kilichokusanywa.
Aidha, amesema kuwa ili viongozi wa kijiji waweze kutoa fedha hizo, ni lazima kuwepo na muhtasari wa vikao vya mikutano ya kijiji unaoeleza matumizi ya fedha hizo katika miradi ya maendeleo ya wananchi. Ameongeza kuwa jukumu la ufuatiliaji wa taratibu hizo ni la mtendaji wa kijiji husika.
