Wazazi watakiwa kutambua umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike
1 April 2024, 18:19 pm
Imeelezwa kuwa chanzo kikubwa kinachosababisha watoto wa kike kutokufikia malengo yao ni wazazi kutotambua umuhimu wa elimu.
Na Musa Mtepa
Wazazi wametakiwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike ili waweze kukabiliana na changamoto za maisha pamoja na kuwa majasiri kwenye kupigania nafasi za uongozi na maamuzi katika jamii .
Hayo yamesemwa 28/3/2024 na mtendaji kata wa kata ya Mkunwa Aron Zephania Parsalaw kwenye mdahalo wa wazi uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mkunwa ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ambapo amesema kuwa suala kubwa linalosababisha watoto wa kike kutofikia malengo yao ni wazazi kutotambua umuhimu wa elimu .
Akichangia mdahalo huo Bw. Musa Liponda mkazi wa kijiji cha Mkunwa amesema kuwa ili mtoto wa kike avuke salama na kufikia umri wa kuwa kiongozi lazima akwepe vikwazo vinavyosababisha mimba za utotoni vilivyoshamiri katika jamii .
Aidha Bw. Liponda ameongeza kuwa mfumo na mitazamo ya malezi iliyopo kwenye jamii imekuwa ikichangia kwa asilimia kubwa kwa mtoto wa kike kutomaliza masomo yake.
Kwa upande wake Vera Assenga mwakilishi kutoka mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) amesema jamii ya wanamkunwa kila mmoja ana jukumu la kuhakikisha anamlinda mtoto wa kike katika kufika malengo yake pamoja na ushiriki wa mwanamke katika nafasi za uongozi na maamuzi.
Naye Coletha Chiponde katibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) Mkunwa amesema jukumu kubwa linalofanywa na kituo hicho ni kuelimisha wazazi na watoto wa kike juu ya umuhimu wa elimu .