Mpanda FM

RC Mrindoko atoa onyo kwa wanaoleta taharuki

6 April 2026, 1:35 pm

Mwanamvua Mrindoko mkuu wa mkoa wa Katavi. Picha na Benny Gadau

“Naomba nisisitize msiamini katika uvumi”

Na Benny Gadau

Mkuu wa Mkoa wa Katavi  Mwanamvua Mrindoko amekemea vikali vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kudhuru wengine kutokana na taarifa zisizo na ukweli, akisisitiza kuwa vitendo vya aina hiyo pamoja na kueneza uzushi havitavumiliwa na serikali.

Mrindoko ametoa kauli hiyo jumapili Aprili 5, 2026, mara baada ya kushiriki ibada ya Pasaka katika Kanisa la Anglikana lililopo kata ya Makanyagio manispaa ya Mpanda.

Amesema baadhi ya taarifa zinazosambazwa mitandaoni na katika jamii hususani zile zenye mwelekeo wa kishirikina na uzushi zimekuwa zikichochea taharuki, hofu na migogoro isiyo ya lazima.

Ameongeza kuwa vyombo vya dola vitaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wote watakaobainika kuhusika katika uenezaji wa taarifa za upotoshaji na uzushi unaosababisha hofu na kuvuruga utulivu wa jamii.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa

Mkuu huyo wa mkoa amewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama katika mkoa wa Katavi ni shwari na kuwataka kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu yoyote.