Mpanda FM
Mpanda FM
4 December 2025, 5:28 pm

Madiwani wa manispaa ya Mpanda. Picha na Samwel Mbugi
“Maadili ndio msingi wa maendeleo yetu katika manispaa yetu ya Mpanda”
Na Samwel Mbugi
Baraza la madiwani la manispaa ya Mpanda mkoani Katavi limempitisha diwani wa kata ya Magamba Charles Philipo kuwa mstahiki Meya baada ya kupata kura 21 kati ya kura zote 21 katika uchaguzi uliofanyika ukumbi wa ofisi ya mkurugenzi.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi ametoa shukrani kwa wajumbe wote waliomuamini kwa kumpigia kura na kuahidi kushirikiana na kila mtu katika kuhakikisha manispaa inapata maendeleo.
Awali zoezi hilo limetanguliwa na viapo vya madiwani ambavyo vilisimamiwa na Rebecca Michael hakimu mkazi mwandamizi mahakama ya wilaya Mpanda.
Hata hivyo mara baada ya kula kiapo mkuu wa kanda ya nyanda za juu kusini anayesimamia maadili ya uongozi Paulo Kanoni amewataka madiwani kuzingatia maadili ya kazi zao kwa mujibu wa sheria za nchi ya Tanzania.
Akizungumza katika Baraza hilo katibu tawala wa mkoa wa Katavi Albert Msovela ambae alikuwa mgeni rasmi amewapongeza madiwani kwa umoja waliouonyesha katika kuchagua uongozi mpya ambapo amewataka kwenda kusimamia miradi ya umma ili kuwezesha halmashauri kuwa na maendeleo.
Baraza hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa mkoa wa katavi.