Mpanda FM
Mpanda FM
5 October 2025, 7:11 pm

Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph akitoa maelekezo kwa wawekezaji. Picha na John Benjamin
“Kuanzia leo nafunga shughuli zote za uchimbaji”
Na John Benjamin
Wananchi wa Kijiji cha Mtisi wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wamelalamikia uwepo wa wawekezaji watatu raia wa kigeni kutoka nchini China wanaojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini katika maeneo ya vyanzo vya maji bila ya kijiji hicho kunufaika.
Wakizungumza wananchi hao wamesema kuwa shughuli hizo za uchimbaji zimeathiri sana vyanzo vya maji vilivyokuwa vikitegemea matumizi ya kila siku ikiwemo maji ya kunywa na kilimo.
Kutokana na malalamiko hayo ya uharibifu imemwibua Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusufu kufika katika maeneo husika na kuchukua hatua za haraka kwa kufunga rasmi shughuli zote za uchimbaji zinazofanyika katika vyanzo vya mto ndani ya kijiji hicho.
Aidha jamila pia ametoa onyo kali kwa wawekezaji wote wanaopuuza taratibu na kushindwa kuwashirikisha wananchi ambapo ameeleza kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kufuta vibali vyao.
Serikali ya wilaya ya Mpanda imeunda timu maalum kwa ajili ya kufanya tathimini ya athari za shughuli hizo kwa mazingira pamoja na kusimamia urejeshaji wa hali ya kawaida kwenye maeneo yaliyoathiriwa.