Mpanda FM
Mpanda FM
2 May 2025, 2:02 pm

Picha ya maandamano siku ya wafanyakazi duniani. Picha na Restuta Nyondo.
“Msikubali kutoa rushwa ya ngono ili kupata haki zenu”
Na Restuta Nyondo
Wafanyakazi mkoani Katavi wamesema bado taasisi na halmashauri zinalegalega katika kulipa madai kwa muda mrefu ikiwemo fedha za likizo,matibabu,uhamisho na fedha za kupandishwa madaraja.
Hayo yamesemwa katika risala iliyosomwa na Katibu wa Chama Cha Walimu CWT manspaa ya Mpanda Pamphilius Abel katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi ambayo kimkoa yamefanyika katika uwanja wa kashaulili halmashauri ya manspaa ya Mpanda.
Amesema changamoto hizo zinaathiri utendaji wa wafanyakazi kwani wamekuwa wakikabiliana na mishahara ambayo bado haitoshelezi ukilinganisha na kupanda kwa gharama za maisha.
Akijibu risala hiyo mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko amezitaka halmashauri zote kulipa madai yote yanayodaiwa bila upendeleo wa kidini, urafiki au ukabila na kuwaasa wafanyakazi kutokubali kudhalilishwa kingono ili kupata haki zao.
Kila ifikapo Mei Mosi Tanzania huadhimisha siku ya wafanyakazi ambapo kitaifa yamefanyika mkoani Singida yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Uchaguzi mkuu 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya wafanyakazi sote tushiriki”.