Chatu awanyima usingizi wakazi wa Kasimba
15 January 2025, 9:36 pm
“Ameonekana tena katika maeneo hayo jioni ya January 15, 2025“
Na Anna Milanzi-Katavi
Wananchi wa mtaa wa Kasimba mkoani Katavi wamejikuta wakiishi kwa hofu kutokana na uwepo wa nyoka aina ya chatu ambaye anaonekana katika maeneo ya Jirani na makazi yao
Chatu huyo ambaye amekuwa akikamata mifugo mbalimbali ikiwemo kuku na mbuzi ameonekana tena katika maeneo hayo jioni ya January 15, 2025 mara baada ya wafugaji kujitoa na kupeleka mifugo katika maeneo hayo ili ibainike uwepo wa chatu huyo endapo atakamata mifugo jambo ambalo limefanikiwa kutokana na Chatu huyo kuua mbuzi mmoja miongoni mwa mbuzi hao
Wananchi hao wameeleza hofu waliyonayo kutokana na uwepo wa chatu huyo huku wakiiomba serikali isaidie kumuondoa chatu huyo
Nae mwenyekiti wa mtaa huo wa Kasimba Benard Nswima amekiri uwepo wa chatu huyo nakueleza namna wananchi walivyojitolea mifugo ili ibainike uwepo wa nyoka huyo ambapo ameeleza hatua alizozichukua mara baada ya kupewa taarifa kuwa chatu ameua mbuzi.
Mkuu wa wilaya ya Mpanda Jamila Yusuph ametembelea katika eneo hilo ambalo chatu anaonekana na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari na kutoa taarifa endapo watamuona nyoka huyo.