Mpanda FM

Waumini wa dini ya Kiislam Katavi watakiwa kujikita katika shughuli za maendeleo

18 June 2024, 8:45 pm

Katika swala ya Eid Al Adha.

“Ibada nzuri ni ile ya kuifikia jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo.”

Na Fatuma Said -Katavi

Katika kusherehekea sikukuu ya Eid Al Adha, Shehe Mkuu wa mkoa wa Katavi Mashaka Kakulukulu, amewataka waumini wa dini ya Kiislam kuachana na mambo maovu na badala yake kujikita katika shughuli za maendeleo.

Kakulukulu amebainisha hayo wakati wa sherehe hizo zilizofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kashato iliyopo Mpanda Mkoani Katavi ambapo amesema kuwa ibada nzuri ni ile ya kuifikia jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Aidha amewataka waumini wanapodhimisha sikukuu za Eid wajikite hasa katika kutekeleza ambayo Mwenyezi Mungu anayataka na sio kwenda kinyume na mafundisho na maadili ya kidini.

Sauti ya Shehe Mkuu wa mkoa wa Katavi Mashaka Omary Kakulukulu

kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko ambaye pia amehudhuria katika sherehe hizo ametumia fursa hiyo kuwaasa waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote kudumisha amani na umoja katika kuleta maendeleo.

Pia amewakumbusha wananchi wote kujiandaa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na uchaguzi Mkuu mwakani, na kuwataka wazazi na walezi kuwafundisha vijana swala la maadili katika jamii zao ili kusaidia kuwa na kizazi kilicho bora.

Sauti ya mkuu wa mkoa akizungumza

Nao baadhi ya waumini wa dini ya Kiislam wafurahia kusherehekea sikukuu hiyo ambapo pia wameiasa jamii kuwa na umoja na mshikamano katika kuleta maendeleo

Sauti za waumini wa dini ya kiislam wakielezea furaha yao kuhusu siku hiyo

Sikukuu ya Eid Al Adha imefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kashato iliyopo Mpanda mkoani Katavi na Kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Mkoa.