Wananchi Katavi wahofia aliyesimamia mgogoro wao na jeshi kuwageuka
17 May 2024, 2:06 pm
Huenda ametugeuka kwa kuwa eneo lake limeachwa wazi hivyo tunadhani kuwa zipo sababu za yeye kuegemea upande mmoja na kusababisha maeneo hayo kuchukuliwa na jeshi” Alisema mmoja wa wananchi aliehudhuria kliniki hiyo. Picha na Lilian Vicent
Na Lilian Vicent -Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko ameendelea na kliniki ya kusikiliza kero ambapo kumeibuka hoja ya mgogoro wa muda mrefu wa mipaka kati ya Jeshi La Wananchi Tanzania [JWTZ] na wananchi wa halmashauri ya Manispaa ya Mpanda.
Hayo yamejiri katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda ambapo mmoja wa Wananchi amesema kuwa kiongozi wao waliomchagua kusimamia mgogoro huo huenda amewageuka kwakuwa eneo lake limeachwa wazi hivyo wanazani kuwa zipo sababu za yeye kuegemea upande mmoja na kusababisha maeneo hayo kuchukuliwa na Jeshi.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa Mwanamvua Hoza Mrindoko amebainisha kwa taarifa aliyonayo mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu tayari umemalizika kwa mujibu wa wataalamu na Wanachi wameshiriki na endapo kuna upande au mtu hajaridhishwa na uamuzi huo aende mahakamani.
Sauti ya mkuu wa mkoa Mwanamvua Hoza Mrindoko akibainisha kuwa taarifa aliyonayo ni kuwa mgogoro huo umekwisha.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amezitaka ngazi zote kuanzia kwa Katibu Tawala Mkoa, halmashauri zote, wakuu wa taasisi na vyombo vya dola kushughulikia kero zote bila kusubiri siku maalum ya kusikiliza kero.
Pia baadhi ya wananchi wamelalamikia baadhi ya viongozi katika ofisi kuwa na tabia ya ubinafsi katika ofisi za umma, ambao Mwanachi mwingine amemwambia Mkuu wa Mkoa kuwa baadhi ya Watumishi wa Umma wanakwamisha mambo kwa makusudi kwani badala ya kusikiliza na kutatua kero za wanachi wamekuwa na tabia ya ‘Umungu Mtu’ kitendo alichokitaja kama kuigombanisha Serikali na wananchi.