Madereva watakiwa kuchukua tahadhari katika msimu wa mvua
1 October 2023, 5:47 pm
Madereva wa magari ya abiria na binafsi mkoani Katavi wametakiwa kuwa makini na kuchukua tahadhari katika kuelekea msimu wa mvua za masika
KATAVI.
Madereva wa magari ya abiria na binafsi mkoani Katavi wametakiwa kuwa makini na kuchukua tahadhari katika kuelekea msimu wa mvua za masika ili kuepuka ajali na vifo vinavyotokana na kutokuwa na umakini kwa baadhi ya madereva .
Baadhi ya mikoa ikiwemo mikoa ya ukanda wa Nyanda za Juu Kusini imetakiwa kuchukua tahadhari kuelekea msimu wa mvua za masika ambazo zinatarajiiwa kuambatana na elnino.
Akizungumza na Mpanda Redio Fm kaimu kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Katavi Geofrey George Mwambungu amesema kuwa kuelekea msimu wa mvua ni vyema madereva wa vyombo vya moto hususani magari kuchukua tahadhari pale wanapoona barabara zimejaa maji na sio kupima kina cha maji kwa macho .
Kwa upande wao madereva wa magari wanaofanya shughuli zao stendi ya zamani iliyopo mji wa zamani kata ya Kashaulili manispaa ya Mpanda wameeleza kuwa ni muhimu kwa dereva anaezingatia kanuni na sheria za udereva kuchukua tahadhari inapotokea hali ya maji kujaa na kufunika barabara ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza kwa kufanya maamuzi yasiyo sahihi.
Hivi karibuni Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa angalizo kwa baadhi ya mikoa ikiwemo mikoa ya ukanda wa Nyanda za Juu Kusini kuchukua tahadhari kuelekea msimu wa mvua za masika ambazo zinatazamiwa kuambatana na elnino.