Kituo cha afya Kazima chaanza kutoa huduma
10 July 2023, 10:30 am
MPANDA
Mkuu wa mkoa wa Katavi Mhe Mwanamvua Mrindoko amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi halmashauri ya manispaa ya Mpanda.
Moja ya miradi iliyotembelewa ni kituo cha afya Kazima kilichojengwa kwa fedha za tozo za miamala ya simu.
Katika ziara hiyo mkuu wa mkoa amewataka wananchi wa kata ya Kazima na maeneo jirani kuanza kukitumia kituo cha afya Kazima kwani tayari kimeanza kutoa huduma baada ya ujenzi wake ulioanza Julai 20, 2022 kwa gharama ya shilingi milioni 250 kukamilika.
Akitoa taarifa ya kituo hicho, mganga mfawidhi kituo cha afya Kazima Dr. Herman Kimango amesema huduma zilianza kutolewa rasmi Juni 19, 2023 kikiwa na watumishi wawili kwa kuanza kutoa huduma za baba, mama na mtoto na huduma ya kliniki.
Aidha Mrindoko amesema changamoto zinazokikabili kituo hicho ni pamoja na kukosekana umeme na amemwagiza meneja wa Shirika la Umeme mkoa wa Katavi kwa kusimamiwa na Katibu Tawala mkoa wa Katavi kuhakikisha majengo yote ya vituo vya afya, hospitali za wilaya, shule za msingi na sekondari kuhakikisha ifikapo Julai 30, 2023 ziwe zimeunganishiwa umeme.