Mashindano UMISETA yafungwa Katavi
10 June 2023, 3:29 pm
KATAVI
Wakurugenzi wa halmashauri zote mkoani Katavi wametakiwa kuhakikisha wanasimamia michezo na kuzitengea bajeti idara zote za michezo katika maeneo yao.
Maagizo hayo yametolewa na katibu tawala wa mkoa wa Katavi Hassan Rugwa wakati akifunga mashindano ya Umoja wa Michezo Shule za Sekondari (UMISETA). Amesema wakurugenzi wanapaswa kuziwezesha idara za michezo kwa kuzipatia vifaa na raslimali fedha ili kukuza sekta ya michezo.
Aidha afisa michezo mkoa wa Katavi Caroli Steven amesema mwaka huu kulikuwa na ushindani mkubwa wa kutafuta timu ya kuwakilisha mkoa ikilinganishwa na miaka mingine iliyopita.
Kwa upande wao baadhi ya wanamichezo waliochaguliwa kuwakilisha mkoa wa Katavi katika ngazi ya taifa wamesema wapo tayari kwenda kushindana na kupata ushindi mkoani Tabora.
Mashindano hayo katika ngazi ya taifa yanatarajiwa kuanza Juni 14 mkoani Tabora huku mkoa wa Katavi ukiwakilishwa na wanamichezo 120 katika mashindano hayo.