Mpanda FM

Magogo yapigwa marufuku buchani

26 May 2023, 10:42 am

MPANDA

Wadau wanaozalisha mazao yatokanayo na mifugo mkoa wa Katavi , wametakiwa kufuata sheria, ikiwemo kuboresha usafi katika mabucha, na kuepuka matumizi ya magogo na vyuma vyenye kutu ili kulinda afya ya walaji.

Maagizo hayo yametolewa na Afisa Mfawidhi wa Bodi ya Nyama Kanda ya Magharibi, Joseph Kulwa wakati wakifanya ukaguzi, usajili na utambuzi wa mabucha katika mkoa wa Katavi na kuongeza kuwa vitu walivyobaini ni wafanyabiashara wa nyama kuongeza mabucha bubu ambayo hayajasajiliwa ikiwa ni pamoja na kupima afya zao.

Kulwa amesema pamoja na kubaini changamoto hizo bado wanaendelea kuwapa elimu pamoja na kuzingatia sheria ya tasnia ya nyama namba 10 ya mwaka 2006 ambayo inawataka watambulike kwa kusajiliwa, huku wakibaini mabucha sita ambayo hayajasajiliwa.

Kwa Upande wa wamiliki wa bucha wamewataka wafanyabiashara wa nyama kuacha matumizi ya magogo kwa ajili ya afya za wateja huku msimamizi wa machinjio ya Mpanda Hotel Juma Gilibert, akiainisha changamoto walizokua wanakabiliwa nazo na kuishukuru serikali kuanza hatua za kutatua changamoto hizo.

Zoezi hilo limewafikia wadau 73 walio kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yatokanayo na mifugo ambapo wadau 28 wametozwa faini kwa kukiuka sheria na kanuni za biashara ya uuzaji nyama, wadau 7 wamefungiwa kujihusisha na biashara hiyo na wadau 3 wamepewa onyo huku zoezi hilo likiwa bado linaendelea mkoani hapa.

#mpandaradiofm97.0

#wizarayaafya

#wizarayamifugonauvuvi