DC Mwaipaya azindua rasmi Msangamkuu Beach festival
28 December 2024, 20:45 pm
Msangamkuu Beach festival hii awamu ya nne ya tamasha hili ambapo dhamira ya tamasha hili ni kutangaza utalii wa fukwe na vivutio vilivyopo katika mkoa wa Mtwara
Na Musa Mtepa
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdala Mwaipaya, leo Desemba 28, 2024, amezindua rasmi tamasha la Msangamkuu Beach Festival (Msimu wa Nne) na kuwahamasisha wananchi wa Mtwara kushiriki kikamilifu katika tukio hilo. DC Mwaipaya amesema kuwa tamasha hili linatoa fursa ya kuhamasisha utalii wa fukwe za bahari, kuonyesha fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii, na kuchangia katika kuhamasisha utalii wa ndani. Amesisitiza kuwa utalii haupaswi kuhusishwa na wageni pekee, bali na wananchi wa ndani pia.
Aidha, DC Mwaipaya ameongeza kuwa tamasha hili linahusisha michezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na michezo ya ufukweni, mpira wa miguu, mashindano ya kuogelea, na masumbwi, pamoja na burudani kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya mkoa wa Mtwara.
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara, Bi. Nanjiva Nzunda, ameeleza kuwa tamasha hili linajivunia kutoa mchango mkubwa katika kukuza utalii wa fukwe, lakini pia linasaidia kujenga umoja, upendo, na utulivu miongoni mwa jamii, na kuhamasisha watu kuwa na mtindo mpya wa kufanya kazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Msangamkuu Beach Festival, Athuman Kambi, ameeleza kuwa malengo ya kamati ni kuhakikisha kwamba katika miaka ijayo, tamasha hili linaratibiwa na wafanyabiashara na wajasiriamali ili kupunguza mzigo wa kiutawala wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara.
Tamasha la mwaka huu linatarajiwa kupambwa na burudani kutoka kwa Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Harmonize, pamoja na wasanii wengine kutoka mkoa wa Mtwara.