Msangamkuu Beach Festival kuzinduliwa rasmi 27 Disemba 2024 Mtwara
17 December 2024, 18:25 pm
Na Musa Mtepa
Tamasha la Msangamkuu Beach Festival, linalohamasisha utalii katika mkoa wa Mtwara na kusini kwa ujumla, linatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 27 Disemba 2024 katika fukwe za Msangamkuu. Tamasha hili litapambwa na burudani mbalimbali kutoka ndani na nje ya mkoa wa Mtwara.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, akizungumzia tamasha hilo, amewaalika wananchi wa ndani na nje ya mkoa wa Mtwara kushiriki, akieleza kuwa kutakuwa na matukio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ya mila na desturi za wakazi wa Mtwara pamoja na matukio mengine.
Aidha, Kanali Sawala amesema kuwa dhamira kuu ya tamasha hili ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa wa Mtwara na kukuza fursa za uwekezaji, hasa katika fukwe zilizopo mkoani humo.
Naye, Emmanuel Mwambe, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, amewaomba wananchi kujumuika kwa pamoja kwani kumeandaliwa siku maalum kwa ajili ya mtu mmoja mmoja na familia kwa ujumla.
Brayton Kawiche, Afisa Muhifadhi wa Mji Mkongwe wa Mikindani, amesema tamasha la Msangamkuu linachangia sana kwa mkoa na kwa mtu mmoja mmoja, kwani limekuwa likiwakutanisha watu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara, wasanii, na wanamichezo, hali inayochochea kukuza uchumi na utalii wa Mtwara.