Jamii FM

Diwani Namtumbuka afanya kikao kazi na viongozi wa vijiji, vitongoji

11 December 2024, 00:17 am

Viongozi wa vijiji,vitongoji na wajumbe wa serikali za mitaa wa kata ya Namtumbuka wakiwa katika kikao kazi (Picha na Musa Mtepa)

Hiki ni kikao kazi kilichoitishwa na Diwani wa kata ya Namtumbuka Al-hajji Salumu Lipwelele chenye lengo la kutambuana na kufahamishana majukumu mbalimbali kwa viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na wataalamu wa Idara mbalimbali katika kata hiyo.

Na Musa Mtepa

Leo, Disemba 10, 2024, Diwani wa Kata ya Namtumbuka, Al-hajji Salumu Lipwelele, amefanya kikao kazi na viongozi wa vijiji na vitongoji vinavyopatikana katika kata hiyo. Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kutambuana na kujua majukumu ya kila kiongozi katika utekelezaji wa shughuli zao za maendeleo.

Akizungumza katika kikao hicho, Al-hajji Lipwelele amesisitiza kuwa kutokana na imani kubwa iliyojitokeza kutoka kwa wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, ambapo viongozi wote wa chama cha Mapinduzi (CCM) walichaguliwa, ni muhimu kwa viongozi hao kukutana, wakuu wa idara, na kufahamiana ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unaenda kwa ufanisi.

Sauti ya 1 Al-hajji Salumu Lipwelele Diwani wa kata ya Namtumbuka

Alhajji Lipwelele amewataka wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuwa viongozi wa kweli na kusimamia maendeleo ya kata ya Namtumbuka katika  miradi ya maendeleo inayotekelezwa na pia kutoa taarifa za maendeleo kwa ngazi ya vijiji na vitongoji. Amesisitiza ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na Idara za Serikali ili kufanikisha maendeleo kwa haraka.

Sauti ya 2 Al-hajji Salumu Lipwelele Diwani wa kata ya Namtumbuka
Diwani wa kata ya Namtumbuka Al-hajji Lipwelele akiongoza kikao kazi cha wenyeviti wa vijiji,vitongoji na wajumbe wa halmashauri ya vijiji(Picha na Musa Mtepa)

Vilevile, ametoa wito kwa wataalamu wa idara mbalimbali kushuka hadi ngazi za chini na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna idara zao zinavyofanya kazi, ili kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao.

Sauti ya 3 Al-hajji Salumu Lipwelele Diwani wa kata ya Namtumbuka

Kwa upande wa maafisa kilimo na mifugo, wamempongeza Diwani Lipwelele kwa jitihada zake za kuandaa kikao hicho na wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao.

Sauti ya Joseph Upendo na Neema Kwayu maafisa kilimo na ufugaji kata ya Namtumbuka
Afisa kilimo kata ya Namtumbuka Neema Kwayu akizungumza mbele ya viongozi wa vijiji na vitongoji(Picha na Musa Mtepa)

Naye, Mwalimu Masumbuko Richard, Afisa Elimu wa Kata ya Namtumbuka, amezungumzia suala la utoro wa wanafunzi katika elimu ya sekondari kwa kusisitiza kuwa viongozi wa vijiji wanapaswa kujitokeza na kuzungumza na wazazi kuhusu umuhimu wa kutokomeza utoro .

Sauti ya Mwalimu Masumbuko Afisa Elimu kata ya Namtumbuka

Baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wamekubaliana na maelekezo hayo na kumpongeza Diwani kwa kuandaa kikao hicho pamoja na kuahidi  kutekeleza yote yaliyozungumzwa na kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuboresha maendeleo ya kata ya Namtumbuka.

Sauti ya baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji kata ya Namtumbuka