Wadau waombwa kuchangia sherehe za Maulid mkoani Mtwara
31 August 2024, 12:21 pm
“Miaka yote tumekuwa tukifanya sherehe hizo kwa kutumia nguvu zetu hivyo kutokana na hali ya maisha kubadilika tunaomba wadau wenye uwezo kuchangia sherehe hizo ili kuendelea kumtukuza Mtume Muhammadi S.W.A”.
Na Musa Mtepa
Umoja wa wanawake waislamu kutoka Chihiko kata ya Mtawanya Manispaa ya Mtwara Mikindani wameomba wadau na jamii ya kiislamu kuchangia sherehe za Maulidi zinazofanyika kila mwaka katika eneo ili kuendeleza kulitukuza jina la Mtume Muhammadi S.A.W.
Wakizungumza na Jamii fm Radio August 25,2024 Wanawake hao wamesema ni zaidi ya miaka 35 sherehe hizo zimekuwa zikifanyika ambapo kwa kipindi cha hivi karibuni wamekuwa wakikutana na changamoto ya kiuchumi hali inayowalazimu kulima vibarua mashambani ili kupata fedha itakayo wasaidia kufanikisha sherehe hizo.
Mzee Seif Akaliwaza Msimamizi wa sherehe hizo amesema ni zaidi ya miaka kumi sasa amekuwa nao huku akiomba wafadhili kuwasaidia akina mama hao katika kufanikisha sherehe hizo.
Kwa upande wake Ostadhi Hamisi Chikambu amesema kitendo kinachofanywa na akina mama hao ni katika kuunga mkono kile kilichofanywa na Bi Hadija ambae alikuwa mke wa Mtume Muhammadi SAW baada ya kutoa mali zake zote kwa mumewe ili aweze kuutangaza uislamu kwa uzuri.