Viongozi wa vijiji Mtwara DC wasisitizwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa uwazi
30 November 2024, 08:18 am
Huu ni uapisho uliohusisha viongozi wa serikali za vijiji kutoka katika tarafa ya Mpapura inayounganisha kata ya Kitere,Libobe,Mpapura, na Ndumbwe .
Na Musa Mtepa
Aliyekuwa Afisa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, John Nkoko, amewataka viongozi wa vijiji na vitongoji kuwatumikia wananchi badala ya kujitafutia kipato katika maeneo yao.
Nkoko ameyasema hayo tarehe 29 Novemba 2024, wakati wa zoezi la uapisho lililofanyika katika shule ya Msingi Mpapura kwa ngazi ya tarafa.
Nkoko amesisitiza kuwa nyadhifa za uenyekiti wa vijiji, vitongoji na wajumbe wa halmashauri ya vijiji si ajira za kudumu kama watumishi wa umma. Viongozi wa vijiji wanawajibu wa kusimamia makusanyo ya mapato katika vijiji vyao ili kusaidia uendeshaji wa ofisi za halmashauri ya vijiji na miradi ya maendeleo ya vijiji.
Aidha Nkoko amesema kuwa viongozi wa vijiji wanapaswa kuzingatia kanuni na taratibu za uendeshaji wa halmashauri ya vijiji, ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya vijiji kila robo ya mwaka, kutoa taarifa za mapato na matumizi ya kijiji kwa wananchi.
Naye, Emmanuel Shilatu, Afisa Tarafa ya Mpapura, amewasisitiza viongozi wa vijiji kusimamia miradi ya maendeleo katika vijiji vyao ili ikamilike kwa wakati huku wakitambua kuwa hakuna posho kwa ajili ya kusimamia miradi hiyo.
Baadhi ya viongozi wa vijiji wamesema watasimamia kiapo walichoapa kwa kuzingatia taratibu na kanuni zinazohusu serikali za vijiji, huku wakisisitiza kusimamia ukusanyaji wa mapato, uwazi, uwajibikaji na kuleta maendeleo kwa wananchi wao.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umefanyika tarehe 27 Novemba 2024 na Kwa mujibu wa sheria na kanuni, viongozi wanatakiwa kuapishwa ndani ya siku 14. Halmashauri ya Mtwara Vijijini tarehe 29 Novemba 2024 iliwaita viongozi wote waliochaguliwa kwa ajili ya kuapishwa katika tarafa zao.