Jamii FM
Jamii FM
30/03/2026, 18:21

Je, viongozi huzaliwa au hutengenezwa na mazingira? Makala hii inachunguza mjadala huo kupitia Mariam Chibwalo, mwanamke aliyethubutu kusimama pekee yake dhidi ya wanaume tisa katika kinyang’anyiro cha udiwani. Akiwa amesukumwa na changamoto na hamasa ya kuwa sauti ya wananchi wa Chuno, Mariam anaonesha kuwa uongozi si ndoto tu bali ni uamuzi wa kusimama na kuwatumikia wengine.
Na Mwanahamisi Chikambu na Mwanaidi Kopakopa.
Nadharia za uongozi duniani zimegawanyika katika makundi mawili makuu. Kuna wanaoamini kuwa viongozi huzaliwa na wengine wanaosisitiza kuwa viongozi hutengenezwa na mazingira au matukio wanayokutana nayo maishani.
Wanaodai viongozi huzaliwa huamini kuwa kipaji cha kuongoza kimo ndani ya damu ya mtu tangu kuzaliwa. Kwa upande mwingine, wanaoamini kuwa mazingira humjenga kiongozi wanasema kuwa changamoto, kero na dhuluma ndizo humsukuma mtu kusimama kidete na kusema ”Sasa basi, mimi nitakuwa sauti ya wenzangu”.
Safari ya uongozi wa Mariam Chibwalo haikuwa nyepesi. Katika kinyang’anyiro cha udiwani, alijitosa akiwa mwanamke pekee akishindana na wanaume tisa. Wengi waliutafsiri ujasiri wake kama ndoto isiyowezekana, lakini kwake yeye, haikuwa tu siasa bali ilikuwa ni wito wa dhati wa kuwatumikia wananchi wa Chuno.