TFS yaombwa kutoa elimu ya huduma za misitu
29 March 2024, 17:46 pm
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wameombwa kutembelea vijiji na kutoa Elimu kwa Wananchi ili wapate uelewa juu ya athari zinazo weza kujitokeza kutokana na matumizi mabaya ya Mazao ya Misitu
Na Musa Mtepa
Akizungumza na Jamii Fm Radio 28/3/2024 Mwenyekiti wa kijiji cha Nyengedi Halmashauri ya Mtwara vijijini Bw Salumu Mtunuma amesema kuwa ili wananchi wapate uelewa juu ya athari hasi za matumizi mabaya ya misitu TFS wanatakiwa kwenda vijijini na kutoa elimu kwa Wananchi na sio kusimama kwenye Vizuizi vya Barabarani na Mitaani kukamata wauazaji wa mkaa.
Aidha Bw Mtunuma amesema kuwa hali ya Mazingira vijijini sio mzuri kutokana na Watu kuingia kwenye Biashara ya mkaa kunakosababisha kupoteza miti na misitu mikubwa pamoja na kupoteza vyanzo vya Asili vya maji .
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Namahyata Shuleni Azizi Mbotani amesema kukusanya Wananchi wengi kwa wakati mmoja kunaweza kuwa na gharama kubwa hivyo serikali na TFS wanaweza kutoa Elimu kwa Wenyeviti na Watendaji wa vijiji ili wao waweze kuwaelimisha Wananchi katika mikutano yao.
Kwa upande wake Peter Christopha Nguyenje Muhifadhi Mwandamizi kutoka ofisi ya wakala wa huduma ya misitu (TFS) Wilaya ya Mtwara amesema kuwa misitu ni mali ya watu wote hivyo ni jukumu la kila mmoja kutunza na kusimamia ili kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoweza kujitokeza.