Jamii FM
Jamii FM
29 January 2026, 18:30 pm

Wazazi na walezi mkoani Mtwara wametakiwa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu katika kipindi hiki cha uandikishaji wa Elimu ya Awali na Msingi. Wito huo umetolewa na MERODI kupitia Jamii FM, ikisisitiza elimu jumuishi, ushirikiano wa jamii na msaada wa serikali kwa wazazi wa watoto wenye ulemavu
Na Musa Mtepa
Wazazi na walezi mkoani Mtwara wametakiwa kuweka kipaumbele katika elimu kwa watoto wenye ulemavu kwa kuhakikisha wanawaandikisha katika kipindi hiki cha uandikishaji wa Elimu ya Awali na Msingi kinachoendelea kote nchini.
Wito huo umetolewa leo Januari 29, 2026 na Frances Chiwango, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na watu wenye ulemavu mkoani Mtwara ya Mtwara Economic Rights Organization for Disabled (MERODI), alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio.
Akizungumza katika kipindi hicho, Chiwango amesema licha ya kuwepo kwa mwamko kwa baadhi ya wazazi na walezi ikilinganishwa na miaka ya nyuma, bado juhudi zaidi zinahitajika ili kuendelea kuwahamasisha wazazi kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu.
Aidha, Chiwango amesema uamuzi wa serikali kuweka mkazo katika elimu jumuishi umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza unyanyapaa kati ya wanafunzi wenye ulemavu na wasio na ulemavu, akitolea mfano safari yake ya kwanza kuelekea shuleni.
Vilevile, ametoa wito kwa viongozi wa serikali za mitaa pamoja na maafisa ustawi wa jamii kushirikiana kwa karibu na wazazi na walezi ili kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata haki yao ya msingi ya elimu.
Kwa upande wake, Maximilian Makau, mdau wa elimu na mjumbe wa Bodi ya MERODI, ameitaka jamii kuacha kuwaona watoto wenye ulemavu kama mzigo, akisisitiza kuwa wana uwezo wa kujitegemea na kufanikiwa kama watu wengine endapo watapatiwa fursa sawa.
Makau pia ameitaka serikali kuwaangalia kwa jicho la pekee wazazi wenye watoto wenye ulemavu, hususan kwa kuwawezesha kupitia mikopo au programu maalumu kama ilivyo kwa makundi mengine maalumu, ili kuwasaidia watoto hao kupata elimu bora.
