Bilioni 114.5 zaboresha sekta ya elimu mkoani Mtwara
28 July 2024, 00:27 am
Maadhimisho ya juma la Elimu huambatana na tathmini ya ufaulu ,kutoa mrejesho kwa wadau wa elimu kuhusu mafanikio na changamoto zake Pamoja na kushirikisha wadau wa elimu kuona ,kutambua na kuthamini kazi za walimu na wanafunzi shuleni.
Na Musa Mtepa
Serikali imetoa zaidi ya Bilioni 114.5 katika kipindi cha miaka mitatu kwa ajili ya maendeleo katika sekta ya Elimu mkoani Mtwara.
Hayo yamesemwa leo July 27, 2024 na mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala kwenye kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu liliofanyika katika viwanja vya Mashujaa mjini Mtwara ambapo amesema kuwa kati ya hizo shilingi Bilioni 76.6 ni kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya Elimu na kiasi cha Bilioni 37.9 kwa ajili ya kugharamia Elimu Msingi bila malipo na vinginevyo.
Aidha Kanali Sawala amesema mkoa wa Mtwara umeendelea kudumisha utamaduni wa kuadhimisha juma la Elimu na kutoa tuzo mbalimbali ikiwa ni sehemu ya hamasa kwa Shule ,Walimu ,Wanafunzi wanaofanya vizuri Pamoja na kutambua mchango wa wadau wengine wanaochangia uboreshaji wa sekta ya Elimu katika mkoa wa Mtwara.
Kwa upande wake mkuu wa utumishi Jeshini Meja Jenerali Marco Gaguti mgeni mwalikwa ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa mkoa wa Mtwara katika hotuba yake amewashukuru wanamtwara kwa mwaliko wa kuhudhuria maadhimisho hayo huku akiwapongeza viongozi kwa maendeleo makubwa wanayofanya katika nyanja mbalimbali .
Naye afisa Elimu mkoa wa Mtwara John Lupenza amesema kuwa katika kuboresha hali ya Elimu kumekuwepo na changamoto katika ufuatiliji na usimamizi wa ufundishaji na ufunzaji kwa baadhi ya mamlaka ya serikali za mitaa kutofanyika ipasavyo Pamoja na baadhi ya wazazi kutoshiriki kikamilifu katika usimamizi na uwezeshaji wa Watoto katika masomo.
Maadhimisho ya juma la Elimu 2023/2024 yameenda sambamba na ugawaji wa zawadi ya Baiskel,Vyeti,Fedha,pikipiki na Kompyuta kwa waliofanya vizuri katika kipindi hicho.