Jamii FM

WAJIFUNGUA KWA TOCHI MTWARA

28 June 2021, 06:29 am

Na Karim Faida

Wanawake wa kijiji cha Kilombero kata ya Mahurunga mkoani Mtwara wameiomba serikali kuwawekea umeme katika Zahanati ya kijiji hicho kwa kuwa wanapitia mazingira Magumu ya kujifungualia kwa mwanga wa tochi za simu majira ya usiku na nguzo zimefikishwa mpaka mbele ya jengo hilo.

nguzo ya Umeme mbele ya Zahanati hiyo

Akiongea na Jamii fm radio Bi Sofia Mdinye ambaye ni mkazi wa kijiji hicho amesema Aprili Mwaka huu amejifungua watoto Mapacha saa sita usiku ambapo amejifungulia nje ya Zahanati hiyo wakati wakimsubili mhudumu na hapakuwa na mwanga wowote na baadae alihamishiwa ndani ya zahanati hiyo na mhudumu alipowasha taa ya sola ilikuwa na mwanga hafifu ambapo mama wa Bi sofia alilazimika kuwasha tochi ya simu yake ya Mkononi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kilombero Ndugu Elias Kandila akizungumza na Karim Faida

Nae Bi Hadija Mwale mkazi wa kijiji hicho amesema kweli ndani ya zahanati hiyo kuna taa ya sola ambapo siku alipompeleka mdogo wake kujifungua palikuwa na mwanga hafifu na alilazimika kuwasha tochi ya simu yake pia.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Ndugu Elias Kandila amesema tayari taarifa hiyo ameifikisha kwa Diwani wa kata ya Mahurunga ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mtwara Mh Selemani Nampanye na amekili kupokea taarifa hiyo na tayari amemfikishia DMO na ameahidi ndani ya wiki hii ataifanyia kazi.

Mhandisi Fadhili Chilombe, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Mtwara.

Kwa upande wake Injinia Fadhili Chilombe ambae ni Meneja wa Tanesco mkoa wa Mtwara amesema inashangaza kuona nguzo za umeme zimefikishwa mpaka mbele ya jengo hilo huku zahanati hiyo ikikosa huduma hiyo muhimu na ameahidi kulifanyia kazi kwa haraka kwa kuwa serikali kupitia mradi wa Ujazilizi ambao utagharimu Tsh Bilioni 300 huku Mtwara wakitakiwa kupata Bilioni 94 utazinduliwa mwezi wa nane huku Kijiji cha Kilombero kikipewa kipaumbele.

Sikiliza makala maalum kuhusu zahanati hiyo