Jamii FM
Jamii FM
28/02/2026, 17:05

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi wa bomba la gesi Ntorya–Madimba ifikapo Septemba 2026
Na Musa Mtepa
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa uchimbaji na ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi asilia kutoka Ntorya kwenda Madimba mkoani Mtwara kukamilisha mradi huo kwa wakati, ili kuendana na mahitaji ya Watanzania.
Rai hiyo ameitoa Februari 27, 2026, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa uchimbaji na usambazaji wa bomba la gesi asilia uliofanyika katika eneo la Ntorya, lililopo kijiji cha Namahyakati Barabarani, kata ya Nanguruwe, mkoani Mtwara.
Ndejembi amesema lengo la wizara ni kuhakikisha kuwa ifikapo Septemba 2026, visima hivyo vinaanza kuzalisha gesi na kuungwa katika bomba kuu la Madimba. Amesisitiza kuwa mkandarasi hana budi kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa wakati na kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa.

Aidha, Ndejembi amesema ili kufanikisha hilo kunahitajika usimamizi wa hali ya juu kutoka kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa kuwepo eneo la mradi muda wote, ili wakati utakapofika mradi huo uweze kuanza kama ilivyopangwa.

Akizungumzia hali ya utekelezaji wa mradi huo, Mjiolojia Mwandamizi ambaye pia ni Meneja wa Mradi wa Ntorya kwa upande wa mkondo wa juu, Patrick Kabwe, amesema utekelezaji ulianza mwaka 2005 baada ya kusainiwa kwa mkataba kati ya TPDC, Ndovu Resources ya Uingereza pamoja na Wizara ya Nishati na Madini kwa wakati huo.
Amesema mwaka 2010 walichimba kisima cha Ntorya namba moja na kufanikiwa kugundua gesi ambayo sasa inatarajiwa kuchimbwa na kuungwa katika bomba kuu la Madimba.

Akimkaribisha Waziri wa Nishati, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. James Mataragio, amesema kitalu cha gesi cha Ntorya ni kitalu kipya kitakachoongeza upatikanaji wa gesi, huku mahitaji yake yakiendelea kuongezeka siku hadi siku kutoka kwa wananchi.
Ameongeza kuwa Wizara ya Nishati kupitia TPDC imejipanga kuhakikisha inachimba na kuzalisha gesi ya kutosha kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kukidhi mahitaji ya viwanda na matumizi ya wananchi.

Kukamilika kwa visima vitatu vya gesi vinavyochimbwa katika eneo la Ntorya — Ntorya namba moja, Ntorya namba mbili na Ntorya namba tatu — kunatarajiwa kuongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa takribani futi za ujazo milioni 60 kwa siku katika uzalishaji wa gesi nchini.
Baada ya uzinduzi huo, Waziri wa Nishati alitembelea eneo la Mnazi Bay, ambapo kuna uchimbaji wa kisima kipya ambacho kikikamilika kitaongeza takribani futi za ujazo milioni 45 za gesi asilia kwa siku. Kwa sasa, uzalishaji wa gesi kutoka Mnazi Bay ni takribani futi za ujazo milioni ni 90 – 100 za gesi asilia kwa siku (Million Standard Cubic Feet per Day) MMscf/d).