Mila, desturi kikwazo wanawake kushiriki nafasi za uongozi Mtwara
27 March 2024, 17:00 pm
Mila na desturi potofu zimekuwa zikiwarudisha nyuma wanawake wengi wilayani Mtwara kushiriki katika nafasi za uongozi na uamuzi na kupelekea kuwa wachache katika ushiriki kwenye vikao vya uamuzi.
Na Musa Mtepa
Imeelezwa kuwa mila na desturi zinazofanyika katika jamii ndicho kikwazo kikubwa kwa wanawake wengi wialayani Mtwara kutoshiriki katika nafasi za uchaguzi na uongozi hali inayopelekea kuwa wachache katika vikao vya maamuzi.
Hayo yameelezwa 26/3/2024 na Bi Habiba Chiwalila mkazi wa kijiji cha Nanyati Halmashauri ya wilaya Mtwara mkoani Mtwara katika majadiliano ya mila na desturi potofu zinazomrudisha nyuma mwanamke kushiriki katika nafasi za uongozi na maamuzi yaliyoandaliwa na shirika la mtandao wa jinsia Tanzania TNGP ambapo amesema kuwa mfumo dume uliotapakaa katika jamii nyingi unaomweka mtoto wa kike nyuma ndio kikwazo kushiriki katika nafasi za uongozi na maamuzi.
Aidha Bi Habiba ameongeza kuwa kitendo cha Wanaume kuwaachia Wanawake majukumu mengi ya kuhudumia familia kama vile kulea watoto,huduma za afya pamoja na huduma ya kuteka maji huchangia Mwanamke kutoshiriki katika mikutano ya maamuzi inayofanyika katika vijiji.
Kwa upande wake Shekhe Mvita Bin Musa mkazi wa kijiji cha Kawawa amesema kuwa karibia Dini zote zina ruhusu mtoto wa kike kuwa kiongozi huku akitoa tahadhari ya kuwa Mwanamke ameumbwa kuwa dhaifu hiyvyo ni rahisi kushawishika akiwa kiongozi.
Pia Shehe Mvita amesema kuwa ili kuondoa changamoto ya kutojiamini na kutoshiriki katika nafasi za uongozi na uamuzi ni vema jamii ikawekeza katika Elimu kwa mtoto wa kike.
Naye Bi Rebecca Kisenha Mwezeshaji kutoka shirika la Mtandao wa jinsia Tanzania TNGP amesema kuwa jamii haina budi kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zimekuwa zikileta matokeo hasi kwa mtoto wa kike katika kufikia malengo yake katika Elimu pamoja na kutoshiriki katika kupigania nafasi za uchaguzi ,uongozi na maamuzi.