RC Sawala ahimiza wananchi Mtwara kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
26 November 2024, 22:09 pm
November 27, 2024 ndio uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajia kufanyika ambao kwa siku za hivi karibuni wananchi wameshuhudia wagombea wakinadi sera zao ikiwa njia ya kuwashawishi kuwachagua katika uchaguzi huo.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa mkoa wa Mtwara wametakiwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika kesho, Novemba 27, 2024, kote nchini.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Novemba 26, 2024. Kanali Sawala amesema kuwa wananchi wote waliyojiandikisha na wana sifa za kupiga kura wanapaswa kutumia nafasi hii muhimu na adhimu ya kupiga kura kesho, ili kuchagua viongozi watakaoweza kuleta maendeleo kwa wananchi.
Aidha, Kanali Sawala ametumia nafasi hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wa Mtwara kwa kushiriki kwa amani na utulivu katika mchakato mzima wa uchaguzi wa serikali za mitaa, kuanzia ulipoanza hadi sasa, huku akisisitiza kuendelea na hali hadi uchaguzi huo utakamilika kesho.
Kwa upande mwingine, kaimu Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Jamaldini Salimu Chamwi, amewahimiza wananchi wote wenye sifa ya kushiriki katika uchaguzi huo,kwa kuwa uchaguzi huo ni muhimu kwakuwa unaanzia katika ngazi ya chini, ambapo viongozi watakaochaguliwa ndio watakaowakilisha maslahi ya wananchi katika mitaa, vijiji, na vitongoji