Jamii FM
Jamii FM
26 September 2025, 11:03 am

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa mafunzo kwa waandishi wa habari mkoani Mtwara, ikiwataka kuzingatia maadili ya taaluma, haki za binadamu na misingi ya utawala bora, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Waandishi wameahidi kutumia mafunzo hayo kuboresha uwajibikaji katika kazi zao
Na Musa Mtepa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imewataka waandishi wa habari mkoani Mtwara kutekeleza majukumu yao kwa weledi, kwa kuzingatia maadili ya taaluma na kuheshimu misingi ya haki za binadamu.
Akizungumza wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari yaliyofanyika September 25, 2025 mjini Mtwara, Afisa Uchunguzi Mkuu kutoka Tume hiyo, Bi. Juliana Laurent, amesema waandishi wa habari ni kiungo muhimu katika mnyororo wa ukusanyaji na upashanaji wa taarifa kwa umma.

Aidha, Bi. Juliana amebainisha kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwakumbusha waandishi habari umuhimu wa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika kazi zao za kila siku, hasa wakati huu taifa linapoelekea katika kipindi muhimu cha uchaguzi.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara, Bw. Bryson Mshana, amesema mafunzo hayo yamekuwa chachu kwa waandishi wa habari kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuimarisha mahusiano kati yao na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na elimu waliyopata na kuahidi kuzingatia mafunzo hayo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
