Wananchi wasisitizwa kushiriki kikamilifu uchaguzi serikali za mitaa
26 September 2024, 17:44 pm
Uchaguzi wa Serikali za mitaa kote nchini unatarajiwa kufanyika Novemba 27,2024 ambapo kwa mujibu wa kanuni Wakurugenzi wa halmashauri ndio wasimamizi wakuu wa uchaguzi huo.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wametakiwa kushiriki kikamilifu katika michakato ya uchaguzi ili wawe na sifa ya kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Wito huu umetolewa leo, Septemba 26, 2024, na Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Mwalimu Hassani Nyange, katika kikao cha kutoa maelekezo kwa viongozi mbalimbali kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa, kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Sekondari ya Mtwara Ufundi.
Mwalimu Nyange amesema kuwa kujiandikisha katika Orodha ya Wapiga Kura ni hatua muhimu ambayo inawapa wananchi wenye sifa haki ya kisheria kushiriki katika uchaguzi, iwe kama wapiga kura au wagombea katika nafasi za uongozi.
Aidha, Mwalimu Nyange amesisitiza kuwa wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wenye umri wa miaka 18 au zaidi na wanaokidhi matakwa kisheria wanapaswa kuhamasishwa kushiriki katika uchaguzi, aidha kwa kuchagua au kuchaguliwa.
Mwanahamisi Libubulu, Diwani wa Viti Maalumu (CCM) Manispaa ya Mtwara Mikindani, na Saidi Issa Kulaga, Katibu wa Chama cha CUF wilaya ya Mtwara, wamesema wamepokea maelekezo haya kwa mikono miwili na kwamba ni wajibu wao kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa.
Nao Viongozi wa dini wamesisitiza umuhimu wa serikali kutoa elimu juu ya umuhimu wa wananchi kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kwakuwa huduma mbalimbali zinaanzia kupatikana kupitia viongozi wa chini wa mitaa na vitongoji.