Mmoja ahofiwa kupoteza maisha kwa kuliwa na mamba mto Ruvuma
26 September 2024, 14:31 pm
Katika kipindi cha miaka miwili inasemekana ni zaidi ya watu wanne wameripotiwa kupoteza maisha kwa kushambuliwa na mamba katika eneo la Kiyongo hali inayoendelea kuhatarisha uhai wa wakulima na wavuvi wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo.
Na Musa Mtepa
Mtu mmoja, Mwasiti Hamisi Saidi (20), anadhaniwa kupoteza maisha baada ya kushambuliwa na mamba katika mto Ruvuma, eneo la Kiyongo, kijiji cha Kitunguli, kata ya Mahurunga, Halmashauri ya Mtwara, mkoani Mtwara.
Akizungumza na Jamii FM Redio tarehe 25 Septemba 2024, Fatuma Malagila ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Jumatatu, tarehe 23 Septemba 2024, walipokwenda kuchota maji mtoni ambapo wakiwa eneo hilo, walipata wazo la kuoga, ndipo mmoja wao akashambuliwa na mamba.
Abasi Mshamu, baba mdogo wa Mwasiti, amesema kwamba baada ya kupata taarifa ya tukio hilo, walijitahidi kuutafuta mwili wa ndugu yao usiku na mchana bila mafanikio.
Aidha kwa upande wa wakulima wanaofanya shughuli zao katika eneo hilo wameeleza kuwa walitoa taarifa kwa ndugu wa karibu wa binti huyo na kuanza mchakato wa kutafuta mwili wake huku wakitoa wito kwa serikali kuangalia tatizo la mamba katika maeneo hayo.
Kwa niaba ya Mwenyekiti wa kijiji cha Kitunguli, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitunguli Shuleni, Bw. Saidi Zuberi Mohamedi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na amewataka wananchi wanaofanya shughuli za kilimo na uvuvi kuchukua tahadhari dhidi ya mamba.