DC Munkunda awataka wananchi kudumisha muungano
26 April 2024, 20:50 pm
Faida za muungano wa Tanganyika na Zanziba ni nyingi kwa pande zote mbili zikiwemo za kibiashara,Uchumi na kijamii.
Na Musa Mtepa
Mkuu wa wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda amewaomba wananchi kuwa wamoja katika kuuenzi na kudumisha muungano wa Tanganyika na Zanziba ili kuendeleza fikra na dhamira za waasisi wa muungano huo.
Hayo ameyasema leo tarehe 26/4/2024 kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya muungano wa Tanganyika na Zanziba yaliyofanyika kiwilaya kwenye viwanja vya Mashujaa mjini Mtwara ambapo mkuu wa wilaya huyo amesema kuwa hata kwenye vitabu takatifu hakuna sehemu iliyoandikwa nendeni mkatengane zaidi ya kusisitiza umoja na kuwa kitu kimoja.
Aidha mkuu wa wilaya ametumia maadhimisho hayo kuwataka vijana wa Mtwara kuchangamkia fursa ya uwepo wa wageni na safari za Kwenda Comoro kujiinua kiuchumi kama serikali ilivyotaka Mtwara kuwa lango la Uchumi kwa mikoa ya kusini.
Wakizungumzia maadhimisho ya muungano Josephat Musa (Mwalimu Maproso) na Mustafa Ali Tulitote wakazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wamesema kumekuwa fursa nyingi zinazo patikana kupitia muungano wa Tanganyika na Zanziba zikiwepo za kibiashara na za kijamii.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26, 1964 ikiwa ni Muungano wa Mataifa mawili huru ya Jamhuri yaTanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambapo kila ifikapo Aprili 26 ya kila Mwaka huadhimishwa.