Jamii FM

Wanawake 78 wajitosa kinyang’anyiro uchaguzi serikali za mitaa Mkunwa

25 November 2024, 17:41 pm

Coletha Titus Chiponde mratibu wa kituo cha taarifa na maarifa mkunwa akifuatilia kwa umakini moja ya mafunzo ya kuwezesha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi(Picha na Musa Mtepa)

Haya ni mafanikio makubwa kwa kata ya Mkunwa na Mtwara kwa ujumla kwa kitendo cha kujitokeza wanawake wengi kugombea katika nafasi mbalimbali za uongozi ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.

Na Musa Mtepa

Zaidi ya wanawake 80 walionesha nia ya kuchukua fomu na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Hadi sasa, wanawake 78 kati yao wamefanikiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kampeni.

Mratibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa kilichopo katika kata ya Mkunwa, Coletha Chiponde, alieleza kuwa mwitikio huu umetokana na elimu inayotolewa na kituo hicho, pamoja na ushirikiano na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia mradi wao wa “Mwanamke na Uongozi.” Elimu hii inawawezesha wanawake kuwa na ufahamu wa haki zao za kisiasa, na kuwahamasisha kushiriki katika uchaguzi.

Sauti ya 1 coletha chiponde mratibu wa kituo cha taarifa na maarifa (KC)

Coletha Chiponde pia amebainisha kuwa kata ya Mkunwa, ambayo ina vijiji sita, imefanikiwa kupata mwanamke mmoja anaye gombea nafasi ya uenyekiti katika Kijiji cha Nyengedi.

Ambapo amesema kuwa  hatua kubwa, kwani hapo awali, hakukuwa na mwanamke aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo ya uenyekiti wa kijiji.

Sauti ya 2 coletha chiponde mratibu wa kituo cha taarifa na maarifa (KC)

Lukia Mnyachi, mgombea pekee wa uenyekiti katika Kijiji cha Nyengedi, ameelezea sababu za kugombea, akisema kwamba moja ya mambo yaliyomvutia ni changamoto ya huduma ya maji pamoja na tatizo la udondokaji wa wanafunzi katika kijiji hicho. Ambapo amesema kuwa, kama atachaguliwa, atajitahidi kuboresha hali ya kijiji hicho.

Sauti ya 1 Lukia Mnyachi Mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika Kijiji cha Nyengedi Mtwara vijijini.

Pia, Lukia ameeleza kuwa katika kipindi hiki cha kampeni, amejiandaa kukabiliana na changamoto za kijinsia zinazoweza kujitokeza, na ametoa shukrani kwa mume wake kwa kumsaidia na kumtia moyo katika safari hii ya uchaguzi.

Sauti ya 2 Lukia Mnyachi Mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika Kijiji cha Nyengedi Mtwara vijijini.

Kwa ujumla, habari hii inaonesha kwamba wanawake katika kata ya Mkunwa wanapigania nafasi za uongozi kwa ujasiri, huku wakichochewa na elimu na uhamasishaji unaofanywa na taasisi kama TGNP.

Hii ni ishara ya mabadiliko makubwa katika ushiriki wa wanawake katika siasa za mitaa.