Kamati ya Bunge yaipongeza Serikali umiliki wa Gesi Asilia
25 March 2024, 14:54 pm
Kamati ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya umma imeipongeza serikali kwa kuchukua hatua ya kuwasomesha vijana wa kitanzania nje ya nchi ambao kwasasa ndio wanao simamia mitambo ya kuchakata na kuzalisha Gesi Asilia katika kjiji cha Madimba Mkoani Mtwara.
Na Musa Mtepa
Kamati ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya umma imesema kitendo cha serikali kuongeza hisa kwenye sekta ya gesi asilia kumefanya nchi kunufaika zaidi na rasilimali hiyo inayotarajiwa kukuza uchumi wa taifa.
Hayo yamebainishwa March 24,2024 na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa mitaji ya umma Deus Clement Sangu,walipotembelea viwanda vya kuchakata Gesi Asilia cha mnazi Bay na Madimba Halmashauri ya wilaya Mtwara mkoani Mtwara.
Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada kubwa za uwekezaji hasa uliofanyika Mwezi Februari, 2024 kwaa kuingia katika rekodi ya nchi ambapo Shirika la Maendeleo ya Petrol nchini (TPDC) imeongeza 20% za hisa na kufanya shirika hilo kuwa na umiliki wa 40% na 60% zinabaki za mwekezaji.
Kwaupande wake Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Vuma Agustino, ameipongeza serikali kuchukua hatua ya kuwasomesha vijana wa kitanzania nje ya nchi ambao kwasasa ndio wanao simamia mitambo hiyo ya kuchakata na kuzalisha gesi.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPDC Balozi Ombeni Sefue amefurahishwa na ujio wa wakilishi hao wa Wananchi katika kuwaonesha jinsi fedha zinavyotumika na mchango unaotolewa kupitia sekta ya Gesi na kusistiza kuwa watahakikisha rasilimali hiyo inatumika katika kubadilisha maisha ya watu pale ambapo Gesi Asilia inapatikana na kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.