Jamii FM
Jamii FM
25 February 2026, 09:42 am

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewahimiza wajasiriamali kuongeza thamani ya bidhaa na kutumia teknolojia, ikiwemo akili mnemba, kukuza biashara zao. Mafunzo hayo yaliandaliwa na SIDO kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwawezesha kibiashara
Na Gregory Millanzi
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, amewataka wajasiriamali kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kuongeza kipato, pamoja na kutumia mitandao ya kijamii kujitangaza na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.
Mwaipaya ameyasema hayo Februari 24, 2026, wakati akifungua semina ya utambuzi wa bidhaa, viwanda na matumizi ya akili mnemba (Artificial Intelligence), iliyofanyika katika Ukumbi wa Benjamini Mkapa, Chuo Kikuu cha MUST Mtwara (zamani Chuo cha Ualimu TTC Kawaida).

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mtwara, Merina Mkuchu, amesema lengo la semina hiyo ni kuwatambua wajasiriamali wa Manispaa ya Mtwara na kuwapatia elimu ya kufanya biashara kidijitali badala ya kufanya biashara kwa mazoea.
Mkuchu ameongeza kuwa kwa sasa wanaandaa kanzidata ya kuwatambua wajasiriamali hao ili kuwaunganisha na wadau mbalimbali wanaofika Mtwara kutafuta washirika wa biashara. Pia, SIDO inaandaa kongani la viwanda katika kila wilaya kwa lengo la kuwaunganisha wajasiriamali na kukuza ushirikiano miongoni mwao.

Naye Afisa Uhusiano kwa Umma kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH), Feisal Abdul, amewahimiza wajasiriamali kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Uendelezaji Ubunifu (Samia Fund), unaolenga kuwajengea uwezo na kuwapatia ruzuku za kuendeleza bunifu zao.

Aidha, kampuni ya Scan Code imetoa mafunzo kwa wajasiriamali wa Mtwara kuhusu matumizi ya Scan Code na akili mnemba katika kujitangaza na kupanua masoko ya biashara zao.
Abdulwahid Khamis, mkufunzi kutoka Scan Code, ameeleza faida za teknolojia hiyo na namna inavyoweza kuwasaidia wajasiriamali kuongeza wigo wa soko na mapato.
