Jamii FM
Jamii FM
24 December 2025, 12:50 pm

Wananchi wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya gesi ya kupikia majumbani ili kuepuka madhara ikiwemo milipuko ya moto
Na Musa Mtepa
Wananchi wameshauriwa kuzingatia matumizi sahihi ya gesi ya kupikia majumbani ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza, ikiwemo milipuko ya moto inayosababishwa na matumizi yasiyo salama ya nishati hiyo.
Ushauri huo umetolewa leo Disemba 24, 2025 na Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Ambros Ndunguru, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Redio.
Ndunguru amesema kuwa, mteja anaponunua gesi dukani, anatakiwa kwanza kuhakikisha anapima uzito wa mtungi wa gesi husika, pamoja na kuzingatia namna sahihi ya kuusafirisha. Ameongeza kuwa baada ya kuufikisha nyumbani, ni vyema kusubiri angalau dakika 30 kabla ya kuanza kuutumia.
Aidha, Ndunguru amesema kuwa kutokana na kuimarika kwa kitengo cha huduma na mawasiliano, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limekuwa likipokea taarifa nyingi kutoka kwa wananchi kuhusu matukio mbalimbali yanayosababishwa na mitungi ya gesi.
Akizungumzia hatua zinazopaswa kuchukuliwa endapo gesi itavuja au kulipuka, Ndunguru amesema kuwa ni muhimu kuepuka kuwasha au kuzima swichi za umeme, pamoja na kuto-buruta kitu chochote chenye uwezo wa kuzalisha cheche, kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha mlipuko mkubwa zaidi.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuzingatia matumizi sahihi ya gesi ya kupikia majumbani, sambamba na kuwasiliana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kupiga simu ya bure 114 kwa ajili ya kupata elimu zaidi au kutoa taarifa za matukio mbalimbali ya uokoaji.
