Jamii FM

Mtwara wapendekeza dira ya maendeleo ya taifa kuangazia mifumo ya elimu

24 July 2024, 07:31 am

Afisa tarafa wa kata ya Ziwani Winfrida Linyembe kwa niaba ya mkuu wa wilaya akiongoza majadiliano ya Dira ya maendeleo ya taifa ya 2025/50 (picha na Musa Mtepa)

Kama sisi tunataka kutengeneza nchi yetu na tunataka kuweka usawa kwenye elimu tutafute namna ambavyo hata hawa waliomaliza digrii wapate hizo nafasi kwenye ajira zinazotoka ,ukiangalia ajira zinazotoka asilimia kubwa ni diploma na certificate digrii ni wachache hivyo zinakatisha tamaa Watoto wanaosoma huko vyuoni.

Na Musa Mtepa

Wadau wa maendeleo wilaya ya Mtwara wameitaka Dira ya taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 /50 itoe kipaumbele katika uwekezaji wa rasilimali watu katika mifumo ya Elimu hasa elimu ya kati ili iweze kuleta  tija na matokeo tarajiwa.

Wakizungumza July 23,2024 kwenye kikao cha ushauri Wilaya ya Mtwara (DCC) kilichofanyika katika chuo cha Ualimu Mtwara (ttc kawaida) kilichojadili na kutathmini Changamoto ya Dira ya taifa ya  mwaka 2020/25 na matarajio ya nini kifanyike katika dira ya taifa ya mwaka 2025/2050.

Mbunge wa jimbo la Nanyamba Abdala Chikota amesema kuwa dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025/2050 inatakiwa kufanya maboresho  katika mifumo ya elimu ambayo ndiyo yenye tija kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla kwakuwa imekuwa ikitengeneza wataalamu na mafundi ambao pia ni sehemu ya tiba ya tatizo la ajira nchini.

Sauti ya Abdala Dadi Chikota Mbunge wa Jimbo la Nanyamba mkoani Mtwara.
Mbunge wa jimbo la Nanyamba Abdala Chikota akitoa maoni katika dira ya taifa ya Mwaka 2025/2050(Picha na Musa Mtepa)

Aidha naye mkurugenzi wa bodi ya Tanzania (CBT) Francis Alfred amesema kuwa matamanio yake ni kuona dira ijayo inatengeneza kada ya elimu kuwa kimbilio kubwa la watu na kuwa moja ya kada inayolipwa mishahara mikubwa ili kuwa na vijana wenye uwezo mkubwa na kuwa program mahususi wa kuwachukua vijana wenye uwezo kuwapeleka kwenye nchi zilizoendelea kiteknolojia kujifunza na kuja kuzifanyia kazi nchini.

Sauti ya Francis Alfred mkurugenzi mtendaji wa bodi ya Korosho Tanzania
Wakuu wa Idara na viongozi wa vyama vya siasa wakifuatilia maoni juu ya dira ya maendeleo ya tifa ya mwaka 2025/2050(Picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake Daktari Maria Manase kutoka chuo cha Afya na Sayansi shirikishi Mtwara (COTC) amesema kupitia dira ya miaka ijayo itengeneze namna ambavyo mtu anasoma nadharia kidogo na sehemu kubwa awe anasoma kwa vitendo ili akifika katika eneo la kazi awe na uwezo mkubwa kulingana na elimu au taaluma aliyosomea.

Sauti ya Daktari Maria Manase kutoka chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mtwara(CPTC)
Daktari Maria Manase kutoka chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mtwara(COTC) akitoa maoni yake juu ya dira ya maendeleo ya taifa ya 2025/2050 (Picha na Musa Mtepa)