CSK: watoa elimu ya ukatili Mtwara vijijini
24 April 2024, 19:42 pm
Matukio ya ukatili wa kijinsia umekuwa ukitokea katika maeneo mbalimbali ya wilayani Mtwara hivyo ndio sababu iliyotufanya kuja kutoa elimu hapa katika Kijiji cha Nanguruwe.
Na Gregory Milanzi
Shirika lisilo la kiserikali la utafiti (CSK) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi dawati la Jinsia na Maafisa wa Ustawi wa Jamii Kutoka Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, wametoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wananchi wa kata ya Nanguruwe.
Elimu hiyo imetolewa kwenye Shule ya Msingi Nanguruwe, Shule ya Sekondari Nanguruwe na kwenye Mkutano wa Hadhara kwenye ofisi ya Kijiji ambapo wametoa elimu ya namna yakukabiliana na Ukatili wa Kijinsia kwa Jamii.
Afisa Uhusiano kwa Umma kutoka CSK Robart Mhando amesema kuwa, wameamua kutoa elimu hiyo baada ya kuwa washindi wa kwanza wa ligi ya Ramadhani ambayo ilifanyika wakati wa Mfungo wa mwezi Mtukufu.
Mhando amesema kuwa, matukio ya ukatili wa kijinsia umekuwa ukijitokeza kwenye maeneo mbalimbali na wameamua kutoa elimu kwenye kata ya Nanguruwe ili kuwafikia zaidi watu wa vijijini.
Nae Afisa Ustawi wa Jamii Kutoka Hospitali ya Nanguruwe Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mariam Kaniki amesema, Elimu hiyo inahitajika sana hasa vijijini kwasababu baadhi wanafanya matukio hayo iwe kwa kujua au kutokujua na kusababisha madhara kwa wanaotendewa hasa watoto na wanawake.
Mkuu wa Dawati la Jinsia Wilaya ya Mtwara Mkaguzi msaidizi wa jeshi la Polisi Juliana Chenge amesema, matukio hayo kwenye jamii yapo na elimi inapaswa kutolewa mara kwa mara na kwa kuona umuhimu huo ametoa wito kwa wananchi pale wanapoona kuna viashiria vya ukatili wa kijinsia pasi wawasiliane na Dawati la jinsia kwa msaada zaidi.