RC Mtwara akabidhi vifaa vya TEHAMA kwa walimu
23 April 2024, 16:58 pm
Vifaa hivi vitasaidia walimu kupakua na kujiongezea maarifa kupitia mtandao ambayo yatasaidia katika kuboresha hali ya ufaulu katika shule zetu
Na Musa Mtepa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala Leo tarehe 23/4/ 2024 amekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa vituo 10 vya walimu (TRC) kupitia Mradi wa Boost vyenye thamani ya shilingi Milioni 343 za kitanzania.
Akikabidhi kwa wawakilishi wa Vituo 10 mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Partick Sawala amewataka kuvitunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa malengo yaliyopangwa ili kuleta matokeo tarajiwa kupitia utendaji kazi katika maeneo yao ikiwemo katika kusaidia na kuwezesha Walimu kujifunza mbinu balimbli za ufundishaji na ujifunzaji kupitia mpango endelevu wa mafunzo ya Walimu kazini (MEWAKA).
Pia Kanali Patrick Sawala amewaelekeza wakuu wa Wilaya kuwa karibu na kwenda kufuatilia kwenye maeneo yao kuona vifaa hivyo vinatumika kama ilivyopangwa au vinginevyo na pia akizitaka Halmashauri zote kuhakikisha zinaajiri walinzi watakao linda vituo vya Walimu (TRC) ambako vifaa hivyo vinaenda kutumika.
Aidha kwa upande wake Mratibu wa mradi wa Boost mkoa wa Mtwara Mwalimu Dadi Ngahalo amesema vifaa hivyo vinaenda kutumika kwenye vituo vya Walimu 10 kwa ajili ya kuboresha mafunzo ya Walimu kazini kupitia mpango Endelevu wa mafunzo ya walimu kazini (MEWAKA)
Naye Shakila Omari Mkwazo na Mohamedi Kazumari maafisa Elimu kutoka kata ya Mitengo na Kilomba wamesema kuwa vifaa hivyo vitawasaidia Walimu katika kuongeza ufaulu kwa Shule mbalimbali kwa kuwa Walimu watakuwa wakipata na kuongeza maarifa mapya kupitia vifaa hivyo.