CBT yashauriwa kuhakiki wakulima kuepuka changamoto za pembejeo
21 December 2024, 14:30 pm
Hiki ni kikao cha ushauri cha mkoa wa Mtwara kinachohusisha uwasilishaji wa taarifa mbalimbali za maendeleo ,changamoto na utatuzi wake ikiwemo katika sekta ya Afya ,Elimu,Uchumi na uzalishaji.
Na Musa Mtepa
Bodi ya Korosho Tanzania imetakiwa kuanzisha mapema uhakiki wa taarifa za wakulima wa zao la korosho ili kuepuka changamoto zinazojitokeza katika zoezi la uandikishaji na ugawaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na serikali kwa wakulima.
Wito huu umetolewa leo, Disemba 21, 2024, na Ismail Liuye, mjumbe wa kikao cha kamati ya ushauri mkoa wa Mtwara na mwenyekiti wa chama cha NCCR – Mageuzi Mkoa wa Mtwara, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu Tawi la Mtwara.
Liuye amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Bodi ya Korosho kuwaeleza wakulima kwa kina kuhusu hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na changamoto zilizojitokeza katika msimu uliopita, hususan kuhusiana na uandikishaji wa mashamba na usimamizi wa pembejeo.
Kwa upande mwingine, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Bw. Mangile Malegesi, amejibu hoja hizo na kusema kuwa wamejipanga kukabiliana na changamoto hizo kwa kuajiri vijana 500 ambao watahusika katika uhuashaji wa taarifa za wakulima, kusimamia usambazaji wa pembejeo, na kutoa elimu kwa wakulima katika vijiji vyote vinavyolima korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani, na Tanga.
Pamoja na majibu hayo wenyevikiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Newala mji , Baisa Abdala Baisa na Yusuph Kateule, wameleza wasiwasi kuhusu mpango huo wa kuajiri vijana kutoka maeneo mingine kuwa hatua hiyo inaweza kupunguza nafasi za ajira kwa vijana wa Mtwara, jambo ambalo litakwamisha maendeleo ya uchumi wa mkoa huo.
Wakati huo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ametoa wito kwa viongozi kuwaambia vijana kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii pindi wanapojitokeza kwa fursa za ajira, ili waweze kunufaika na nafasi hizo.