Wananchi Mtwara washauriwa kuwa na utamaduni wa kupanda miti
21 April 2024, 16:26 pm
Miti na misitu ina faida nyingi kwa maisha ya binadamu ikiwa ni Pamoja na kuwa chanzo cha mvua,dawa ,chakula na ni chanzo cha bidhaa za ujenzi
Na Gregory Milanzi
Wananchi wameshauriwa kuwa na utamaduni wa upandaji wa miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi Pamoja na urejeshwaji wa uoto wa asili uliopotea.
Hayo yamesemwa na afisa mazingira Mkoa wa Mtwara alipokuwa anazungumza na Jamii fm radio ambapo amesema kuwa wananchi hawana budi kuendelea na utunzaji wa misitu Pamoja na upandaji wa miti .
Aidha Masumbuko amesema kuwa upandaji wa miti wananchi wanaweza kupanda miti yenye manufaa ikiwemo ya matunda kama vile mikorosho ,mipapai ambayo inaweza kuwa sehemu ya kilimo na wakati mwingine ikitunza mazingira .
Akizungumzia mikakati ya ofis i ya mazingira mkoa wa Mtwara katika utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti amesema kuwa wanaendelea na uboreshaji na utaratibu wa kuwa na klabu za wanafunzi mashuleni ili baadae wawe msaada mkubwa wa kuelimisha jamii juu ya utunzaji wa Mazingira.
Kwa upande wake afisa Muhifadhi Mwandamizi kutoka ofisi ya Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa wilaya ya Mtwara Peter Christopher Nguyeje ameelezea umuhimu wa uwepo wa miti na misitu katika Maisha ya binadamu kuwa ni Pamoja na upatikanaji wa dawa ,vyakula Pamoja na kusaidia kuzuia mmonyoko wa udongo.
Hata hivyo Peter Nguyeje amesema wamekuwa wakitumia njia mbalimbali za kukabiriana na athari za ukataji wa miti ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu kwa Wananchi kupitia vyombo vya habari juu ya athari ya ukataji holela wa miti .
Shafii Mohamedi Linangwa ni mkazi wa mtaa wa Naliendele Manispaa ya Mtwara Mikindani amesema kuwa ukataji wa miti hovyo umekuwa ukileta athari kubwa kwa upande wa binadamu ikiwepo upungufu wa kiwango cha mvua .
Pia Shafii Linangwa ameiomba serikali kuona haja ya kupunguza bei gesi ya kupikia majumbani ili kuepusha ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa ambao umekuwa ukitumiwa na watanzania wengi kama nishati ya kupikia.