Jamii FM

FPCT Mtwara yawapatia watoto zawadi za Krismasi

20 December 2025, 19:57 pm

Baadhi ya watoto na vijana wanaonufaika na kituo cha maendeleo ya mtoto na vijana cha FPCT Mtwara (Picha na Musa Mtepa)

Kituo cha Maendeleo ya Mtoto na Kijana FPCT Mtwara kimetoa zawadi za Krismasi kwa watoto wanaosoma kituoni hapo, ikiwa ni kuwapongeza na kumshukuru Mungu

Na Musa Mtepa

Kituo cha Maendeleo ya Mtoto na Kijana cha FPCT Mtwara kimetoa zawadi za Krismasi kwa watoto wanaosoma katika Kituo cha Huduma ya Mtoto, ikiwa ni sehemu ya kumshukuru Mungu na kuwapongeza watoto hao kwa juhudi zao katika masomo.

Akizungumza leo Disemba 20, 2025 wakati wa zoezi la utoaji wa zawadi hizo, Mchungaji Kiongozi Msaidizi wa Kanisa la FPCT Mtwara, Frank Mchihama, amesema pamoja na utoaji wa zawadi, kituo hicho kimezindua utaratibu mpya wa ufadhili wa ndani, utakaosaidia kukusanya fedha kwa ajili ya kuwafikia watoto wengine waliopo katika mazingira magumu ambao bado hawajapata fursa ya kuhudumiwa na kituo hicho.

Sauti ya 1: Frank Mchihama, Mchungaji Kiongozi Msaidizi FPCT Mtwara
Mchungaji Kiongozi Msaidizi wa Kanisa la FPCT Mtwara, Frank Mchihama akielezea juu ya uzinduzi wa ufadhili wa ndani (Picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake, Afisa mawasiliano na fedha wa Kituo hicho, Bi Dorcas Mlawa, amesema zawadi zilizotolewa zimegharimu jumla ya shilingi milioni sita. Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya uendeshaji wa kituo, wamepata mafanikio makubwa ikiwemo kuwasaidia watoto kufikia viwango mbalimbali vya elimu kama vile kidato cha sita, vyuo vya kati pamoja na vyuo vikuu.

Sauti ya 1: Dorcas Jackson, Meneja wa Kituo
Afisa mawasiliano na fedha Bi Dorcas Mlawa akielezea juu ya mafanikio ya kituo (picha na Musa Mtepa)

Aidha, Bi Dorcas amesema kituo hicho hakibagui watoto, kwani kinapokea watoto kutoka jamii zote bila kujali imani, rangi au kabila, akisisitiza kuwa kigezo kikubwa ni mtoto kutoka katika mazingira magumu.

Sauti ya 2: Dorcas Jackson, Meneja wa Kituo

Akizungumzia umuhimu wa kufadhili watoto wenye uhitaji, Mchungaji Enoshi Aloyce wa FPCT Mtwara ameitaka jamii kuwa na amani na furaha kwa kushika mkono wa mtoto mwenye uhitaji ili aweze kupata elimu na kujikwamua katika umasikini.

Sauti: Mchungaji Enoshi Aloyce, FPCT Mtwara

Nao baadhi ya wazazi pamoja na watoto wanufaika wa kituo hicho wamekishukuru uongozi wa kituo kwa kuendelea kuwapatia msaada na zawadi mbalimbali. Wametoa wito kwa wazazi na walezi wanaoishi katika mazingira magumu kuwapeleka watoto wao katika kituo hicho ili waweze kunufaika na huduma na misaada inayotolewa.

Sauti za baadhi ya wazazi na watoto wanufaika wa kituo hicho
Mmoja ya miongoni mwa wazazi waliojitokeza wakati wa upokeaji wa zawadi za watoto katika kituo cha maendeleo ya mtoto na vijani FPCT Mtwara(picha na Musa Mtepa)