Uzinduzi wa msimu wa kilimo biashara mkoa wa Mtwara
18 November 2023, 12:44 pm
Wadau wa kilimo kila mmoja anawajibika katika kutekeleza majukumu yake ili kufikia malengo tuliyojiwekea kama mkoa ikiwepo kuondoa changamoto zinazowakabiri wakulima
Na Musa Mtepa
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abasi Novemba 17, 2023 amefanya uzinduzi wa msimu wa kilimo wa mazao ya Biashara 2023/2024 katika kijiji cha Nanyumbu wilayani Nanyumbu.
Akizungumza katika uzinduzi huo mkuu wa mkoa amewataka wadau wa kilimo kila mmoja kuwajibika katika kutekeleza majukumu yake ili kufikia malengo waliyojiwekea kama mkoa ikiwepo kuondoa changamoto zinazo wakabiri wakulima zikiwemo za vyama vikuu, AMCOS, Wananunuzi pamoja na taasisi za fedha.
Aidha mkuu wa mkoa Kanal Ahmedi amewahakikshia wakulima wa mazao ya Biashara yakiwemo Korosho, ufuta, Mbaazi na Karanga kuwa changamoto zinazo wakabili kuzifanyia kazi na matokeo yake kuonekana kwa muda mfupi.
Pia Kanali Ahmed Abasi amewasisitiza wakulima kuongeza uzalisha na tija kwenye mazao ya ziada badala ya kutegemea zao la korosho pekee yake kwani kwa kufanya hivyo kutakuwa na ongezeko la mapato na uhakika wa chakula kwa Wananchi.
Kwa upande wake katibu tawala msaidizi sehemu ya uchumi na uzalishaji Bi Nanjiva Mzunda amesema kuwa katika msimu wa kilimo 2022/23 kumekuwa na ongezeko la mauzo ya Mbazi ukilinganisha na misimu ya nyuma ambapo kwa msimu huu jumla ya tani 17445 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 35 zimeuzwa.
Wakati kwa upande wa zao ufuta ukionesha kuongeza kutoka tani 9524 kwa msimu wa 2021/22 hadi tani 17845 kwa msimu wa 2022/23 ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 66 zimepatikana kupitia zao hilo.
Aidha Bi Nanjiva amesema kuwa msimu wa 2023/24 serikali ya India kupitia Balozi wake nchini wamethibitisha kununua tani laki mbili za mazao ya Mbazi na Choroko kutoka Tanzania hivyo ni fursa kwa mkoa katika kuahamasisha Wakulima kulima kadri wanavyoweza kwa ajili ya kuboresha Maisha yao.