Wakulima wa chumvi Mtwara waipongeza Serikali kwa kuwaboreshea Miundombinu
18 February 2021, 10:14 am
Mapema leo tarehe 17 Februari, 2021 uongozi wa Kikundi cha Vijana cha Makonde Salt kilichopo kata ya Ndumbwe umeipongeza halmashauri ya wilaya ya Mtwara kwa uwezeshaji wa mkopo wa zaidi ya Milioni 15 uliosaidia kuboresha miundombinu ya mashamba yao ya chumvi hali iliyosababisha kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 300 hadi 600 za Chumvi kwa kipindi cha uzalishaji.
Hayo yamesemwa katika eneo la uzalishaji mara baada ya kutembelewa na baadhi ya wataalamu kutoka sekta ya kilimo na maendeleo ya jamii kwa minajili ya kujionea shughuli za uzalishaji wa Chumvi pamoja na kujadiliana namna bora ya kuongeza wigo wa uzalishaji kufikia hadhi ya kiwanda.
Awali akiongea na wataalamu hao mshauri wa kikundi Bwn. John E. Mwanache ametanabaisha kuwa zoezi la uzalishaji linafanyika mara moja kwa mwaka kuanzia mwezi Mei hadi Disemba ambapo mvua zinaanza na maji ya mvua yakichanganyika na ya chumvi katika mabirika ya uzalishaji yanatengeneza tope ambalo linaweza kuzuia chumvi kuzalishwa au chumvi kuwa chafu jambo ambalo linaweza kuwaangusha kibiashara.
Ameendelea kusema kuwa, chumvi inayozalishwa inavunwa ikiwa safi na kuwekwa madini joto pindi inapopelekwa sokoni ikiwa katika vifungashio bora ambapo amebainisha wateja wakubwa wa bidhaa hiyo wanatoka sehemu mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya kaskazini.
Kwa upande wa mdhamini wa kikundi hicho Bwn. Mvita S. Shona amesema kuwa eneo lao lina ukubwa wa ekari 13 zinazofaa kwa uzalishaji na kwakuwa wameshatembelewa na baadhi ya mashirika kama vile SIDO na Mamlaka ya Chakula na Dawa ambao wamewashauri mambo mengi ikiwemo kujenga Ghala lenye hadhi ya kiwanda.
Ameedelea kufafanua kuwa, jambo hilo wameishirikisha halmashauri ambapo mhandisi wa ujenzi ameweza kuwatemebelea na kuwashauri kisha kuwachorea mchoro wa ghala kulingana na mahitaji yao jambo ambalo linazidi kuwapa imani kwa serikali yao, kwa sasa wamejipanga kufanya maombi ya mkopo wa zaidi ya Milioni 30 kwakuwa ule wa mwanzo walishafanikiwa kuulipa kwa wakati.Kikundi cha Makonde Salt, ni moja ya vikundi vya vijana vinavyonufaika na mkopo wa 10% ya makusanyo ya mapato ya ndani.