

17 March 2025, 22:15 pm
Tukio la kujeruhiwa na radi Wanafunzi watatu wa shule ya sekondari Madimba limetokea siku ya Jumanne ya March 11 wakiwa Darasani
Na Musa Mtepa
Wanafunzi watatu wa Shule ya Sekondari Madimba, iliyopo katika Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Mkoani Mtwara, wamenusurika kifo baada ya kujeruhiwa na radi iliyotua katika viwanja vya shule hiyo.
Tukio hili lilitokea siku ya Jumanne, Machi 11, 2025, wakati wanafunzi hao walipokuwa darasani.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Madimba, Bw. Hamdi Hassani Mdumba, ameeleza kwamba radi imejeruhi wanafunzi watatu wa Kidato cha Nne. Wanafunzi hawa walipelekwa katika Zahanati ya Madimba kwa matibabu zaidi .
Katika hatua nyingine, Bw. Hamdi ametoa wito kwa serikali kuangalia njia bora ya kuweka vizuizi au vikinga radi kwenye vyumba vya madarasa, ili kuwalinda wanafunzi dhidi ya madhara ya radi wanapokuwa shuleni hasa wakati wa mvua.
Kwa upande mwingine, Issa Msaka, mzazi wa mmoja wa wanafunzi waliojeruhiwa na radi,amesema kuwa alipata taarifa mtoto wake kujeruhiwa na radi akiwa narejea kutoka shambani ndipo alichukua jitihada za haraka kumpeleka Zahanati kwa ajili ya matibabu.
Wakazi wa Kijiji cha Madimba wameeleza kuwa tukio hili ni la kwanza kutokea katika kijiji chao tangu kuanzishwa kwake, hali iliyowapa mshangao na wasiwasi mkubwa.